Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama ilivyomaliza sakata maziko ya Lungu kwa siku 322

Muktasari:

  • Mgogoro wa mahali atakapozikwa Edger Lungu ulipelekea mwili wake kubaki katika chumba cha kuhifadhi maiti nchini Afrika Kusini tangu alipofariki dunia Juni 5, 2025.

Johannesburg. Ikiwa zimetimia siku 322 leo Aprili 23, 2026 tangu aliyekuwa rais wa Zambia, Edgar Lungu alipofariki dunia, Mahakama Kuu ya Pretoria imekabidhi rasmi mwili wa kiongozi huyo kwa mamlaka ya Zambia.

Mgogoro wa mahali atakapozikwa kiongozi huyo ulisababisha mwili wake kubaki katika chumba cha kuhifadhi maiti nchini Afrika Kusini tangu alipofariki dunia Juni 5, 2025.

Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha amesema mahakama imefikia uamuzi huo baada ya familia ya marehemu kuachana na juhudi za kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Afrika Kusini.

“Mwili wa rais wa zamani tayari umehamishwa kutoka Two Mountains Burial Services hadi katika kituo kinachosimamiwa na serikali ya Afrika Kusini,” amesema Kabesha katika taarifa yake.

Uamuzi huo unatekeleza hukumu ya Mahakama Kuu ya Pretoria ya Agosti 8, 2025, iliyotaka mwili huo ukabidhiwe kwa serikali ya Zambia ili kuruhusu maandalizi ya kusafirishwa na kuzikwa Lusaka.

Kabesha ameongeza kuwa serikali sasa itaanza mazungumzo na familia ya marehemu kukamilisha taratibu za mazishi, huku wananchi wakiahidiwa kupewa taarifa rasmi pindi mipango itakapokamilika.

Edgar Lungu ambaye alikuwa Rais wa Sita wa Zambia aliongoza Taifa hilo kuanzia mwaka 2015 hadi 2021 na kufariki dunia nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kifo chake kilizua mvutano mkubwa kati ya familia yake na serikali ya mrithi wake, Hakainde Hichilema. Familia ilitaka azikwe Afrika Kusini, huku serikali ikisisitiza mazishi ya kitaifa yafanyike Zambia.

Mvutano huo uliathiriwa pia na historia ya uhasama wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili.

Ikumbukwe Hakainde Hichilema aliwahi kufungwa mwaka 2017 wakati wa utawala wa Lungu, huku baadaye Lungu akiishutumu serikali ya Hichilema kwa kumwandama na hata kumzuia kusafiri kwa matibabu madai ambayo serikali iliyakanusha.

Familia ya Lungu iliwahi kueleza hadharani kuwa marehemu hakutaka Hichilema ahusishwe katika mazishi yake.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Pretoria iliamua kuwa matakwa ya familia hayawezi kushinda haki ya taifa kumuenzi kiongozi wake kwa mazishi ya kitaifa.

“Hamu binafsi ya rais wa zamani au ya familia yake haiwezi kuzidi haki ya serikali kumuenzi kwa mazishi ya kitaifa,” ilisema mahakama katika hukumu yake.

Hadi sasa, tarehe rasmi ya kusafirishwa kwa mwili kwenda Lusaka na mazishi ya kitaifa bado haijawekwa wazi.