Hatimaye Lungu kuzikwa Zambia, Mahakama yaamua
Muktasari:
- Mahakama nchini Afrika Kusini imeamua leo kwamba Serikali ya Zambia ina mamlaka ya kufanya mazishi ya kitaifa ya kiongozi wake huyo wa zamani.
Dar es Salaam. Baada ya kizungumkuti cha muda mrefu juu ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu hatimaye Mahakama nchini Afrika Kusini imeamuru mwili wake kurejeshwa nchini Zambia kwa maziko ya kitaifa.
Lungu (68), aliyetumikia kama Rais wa Zambia kutoka mwaka 2015 hadi 2021, alifariki dunia Juni 5, 2025, kutokana na ugonjwa ambao haukuelezwa, wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Awali, kulikuwa na mvutano kati ya familia ya Lungu na Serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Hakainde Hichilema ikiwemo hayati kuacha wosia akieleza kwamba Rais huyo asisogelee mwili wake, pia kutaka kuzikwa kwa siri.
Kwa mujibu wa Abc News, DW na Africa News, Mahakama ya Afrika Kusini imeipa Serikali ya Zambia haki ya kumrejesha nyumbani Lungu kwa mazishi ya Serikali.
Mahakama ya Afrika Kusini imeamua kuunga mkono Serikali ya Zambia na kuiruhusu kurejesha mwili wake, licha ya pingamizi kutoka kwa familia yake.
Uamuzi huo unahitimisha mzozo wa kisheria kuhusu mahali ambapo kiongozi huyo anapaswa kuzikwa, na kuangazia mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na mvutano kati ya matakwa ya kibinafsi na itifaki ya kitaifa.
Leo Ijumaa, Jaji Aubrey Ledwaba wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ameamua kwamba Zambia ilikuwa na haki ya kisheria ya kuendesha mazishi ya kitaifa ya Lungu.
Mahakama imesisitiza kuzikwa kwa kiongozi wa zamani wa nchi ni suala la maslahi ya umma, na kushinda matakwa yoyote ya kibinafsi yaliyotolewa na marehemu au familia yake.
Ikumbukwe Jumatano Juni 25, 2025 Mahakama Kuu ya Afrika Kusini lisitisha mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini humo baada ya Mahakama hiyo kutoa zuio la muda hadi pale kesi ya msingi iliyofunguliwa na Serikali ya Zambia itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Awali, familia ya Lungu ilitoa taarifa ya ujumbe wa marehemu ya kwamba mrithi wake ambaye ni Rais wa sasa, Hichilema asisogelee mwili wake huku ikisema hapaswi kuwa karibu na mwili wake huku akitaka maziko yake yawe ya faragha.
Ingawa Serikali ilikuwa ilipanga kurudisha mwili wake nyumbani, lakini ilishindwa kufanya hivyo kutokana na mzozo na familia ya Lungu na chama chake cha siasa cha Patriotic Front (PF), kuhusu maombolezo na mipango ya mazishi.
Viongozi hao wawili walikuwa wapinzani wa kisiasa kwa muda mrefu ambapo Hichilema alimshinda Lungu katika uchaguzi wa mwaka 2021.
Msemaji wa familia ya Lungu, wakili Makebi Zulu, awali aliiambia BBC kwamba familia haikupinga mazishi ya kitaifa, lakini ilitaka kushiriki kuamua nani ataongoza ibada.