Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dhahabu ya Sh1.2 bilioni yadakwa Dar, wahusika wahojiwa

Muktasari:

  • Dhahabu hiyo ilikamatwa Julai 25, 2026, Kiluvya jijini Dar es Salaam, huku wahusika wakihojiwa na vyombo vya usalama.

Dar es Salaam. Dhahabu yenye uzito wa kilo 4.4 na thamani ya Sh1.238 bilioni imekamatwa Kiluvya jijini Dar es Salaam katika operesheni maalumu ya kukabiliana na utoroshaji wa madini, iliyofanywa na kikosi kazi cha Wizara ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya dola.

Hayo yameelezwa leo, Julai 27, 2026, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Madini, Antony Mavunde, katika mkutano na waandishi wa habari na kwamba Serikali itawachukulia hatua kali wanaojihusisha na utoroshaji wa madini hayo, ikiwemo kufutiwa leseni za biashara na kuzuiwa kufanya shughuli zozote katika sekta hiyo.

“Dhahabu hiyo yenye thamani ya Sh1.238 bilioni ilikamatwa Julai 25, 2026, Kiluvya jijini Dar es Salaam, na vyombo vya dola katika operesheni ya kudhibiti usafirishaji haramu wa madini iliyofanywa na kikosi kazi cha Wizara ya Madini,” amesema Mavunde.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde akionesha dhahabu yenye uzito wa kilo 4.4 na thamani ya Sh1.238 bilioni imekamatwa Kiluvya jijini Dar es Salaam katika operesheni maalumu ya kukabiliana na utoroshaji wa madini.

Amefafanua kuwa baada ya kukamatwa, dhahabu hiyo imehifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa imefungwa lakiri kwa namba za turubai ya madini MC 1066128 na MC 1066129.

Akizungumzia tukio hilo, Mavunde amesema mtu yeyote anayetorosha madini anaikosesha nchi mapato yanayopaswa kutumika kuboresha huduma kwa wananchi, hivyo akawataka wafanyabiashara wote kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Ameonya kuwa madini yoyote yatakayokamatwa yakiwa hayana vibali halali au hayajapitia katika masoko rasmi ya madini, yatataifishwa na Serikali na kuhifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania.

Mavunde amesema uchunguzi unaonesha wahusika wamebadili mbinu za utoroshaji kwa kutumia vyombo vya usafiri kusafirisha madini.

“Mfano, hawa walitumia usafiri wa gari kutoka Kahama hadi Dar es Salaam, na si mara ya kwanza. Jambo hili linaashiria kuna mnyororo wa biashara hiyo.

"Hii si mara ya kwanza. Nimeelekeza kikosi kazi cha madini kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wote wanahojiwa ili kubaini mtu anayepokea madini hayo Dar es Salaam, ambaye anaonekana kuwa chanzo na kichocheo cha mtandao huu wa utoroshaji,” amesema.

Dhahabu yenye uzito wa kilo 4.4 na thamani ya Sh1.238 bilioni imekamatwa Kiluvya jijini Dar es Salaam katika operesheni maalumu ya kukabiliana na utoroshaji wa madini.

Amesema lengo la Serikali si kuwakamata wasafirishaji pekee, bali kuvunja mtandao mzima wa utoroshaji kwa kuwabaini wanaoratibu na kupokea madini hayo.

“Kuwakamata wanaobeba madini si tatizo. Muhimu ni kujua yanapelekwa kwa nani na kutibu mzizi wa tatizo,” amesema.

“Atakayebainika kuhusika atafutiwa leseni na kuwekwa kwenye orodha ya watu wasiostahili tena kufanya biashara wala shughuli yoyote katika sekta ya madini. Hili liwe fundisho kwa wengine,” amesema.

Mavunde amesema hatua za kudhibiti utoroshaji zimeendelea kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi, akibainisha kuwa mwaka wa fedha 2024/25 sekta hiyo iliongoza kwa kuchangia mapato yasiyo ya kodi kwa kuingiza zaidi ya Sh1 trilioni katika Mfuko Mkuu wa Serikali.