Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yaidhinisha ushindi wa Rajoelina

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina

Muktasari:

  • DW imeripoti kuwa Rajoelina (49), ambaye yupo tayari kuanza muhula wake wa pili wa uongozi, amesema ushindi huo ni wa kishindo na kwamba hatoruhusu ukosoaji dhidi yake utakaopelekea machafuko kwa taifa hilo.

Dar es Salaam. Rais wa sasa wa Madagascar Andry Rajoelina ametangazwa mshindi na Mahakama ya Kikatiba nchini humo kuthibitisha matokeo ya uchaguzi.

DW imeripoti kuwa Rajoelina (49), ambaye yupo tayari kuanza muhula wake wa pili wa uongozi, amesema ushindi huo ni wa kishindo na kwamba hatoruhusu ukosoaji dhidi yake utakaopelekea machafuko kwa taifa hilo.

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani zimetoa wito kupunguza mvutano wa kisiasa nchini humo kufuatia mahakama kuidhinisha ushindi huo Desemba Mosi, baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita.

Wagombea 11 wa upinzani wa urais bado wanashikilia msimamo wao wa kutokuyatambua matokeo hayo kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi.

Hata hivyo, Rais huyo, ameeleza kuwa dhamira yake kuu katika kuwajali na kuwathamini watu hasa maskini na ameahidi kuharakisha hatua ya kuruhusu uanzishwaji wa viwanda vipya, vitakavyo toa ajira na kuimarisha uchumi.

Aidha, Rais huyo ameujulisha umma juu ya kusudio lake la kufanya mabadiliko madogo kwenye Serikali, huku akijinasibu kuwa timu ya ushindi haifai kufanyiwa mabadiliko makubwa.

Baada ya mahakama kuhalalisha matokeo hayo, mabalozi kutoka EU na Marekani na nchi nyingine wafadhili wameonesha wasiwasi wao kutokana na mivutano iliyoshamiri wakati na kampeni.

Katika taarifa yao wanadiplomasia hao wamesema, Rajoelina ni lazima afanye juhudi za ziada kurejesha imani itakayotoa nafasi ya mazungumzo, huku wakisisitiza juu ya mapendekezo yao ya mara kwa mara kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi kabla ya uchaguzi ujao. 

Mivutano ya kisiasa imeonekana kushamiri katika kisiwa hicho kwa miezi kadhaa, ambapo makanali wawili wa jeshi wameshtakiwa kwa makosa ya kuchochea uasi kuelekea uchaguzi huo wa Novemba 16.

Mkuu wa Jeshi, William Michel Andriamasimanana amesisitiza juu ya jeshi kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo.

Siteny Randrianasoloniaiko, aliyekuwa mmoja wa wagombea kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais, amefungua kesi mahakamani kupinga uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo.

Randrianasoloniaiko anadai kuwepo kwa uchakachuaji wa matokeo ya urais na ununuzi wa kura.

Ni mara chache mno kwa taifa hilo la kisiwa kufanya uchaguzi bila ya kuwepo kwa mzozo wowote.

Mgogoro wa hivi karibuni uliibuka mwezi Juni, baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Andry Rajoelina alikuwa na uraia pacha wa Ufaransa, na hivyo kusababisha kuibuka kwa hoja ya wapinzani wake kutaka aenguliwe katika nafasi ya kuwania kiti cha urais. 

Rajoelina mwenyewe alikanusha madai hayo na kujitetea kuwa, alichukua uraia wa Ufaransa ili kuruhusu watoto wake kusoma nje ya nchi.

Kabla ya uchaguzi, wagombea wa upinzani walifanya maandamano karibu kila siku katika mji mkuu, Antananarivo huku maandamano hayo yakitawanywa na vikosi vya usalama kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.

Rajoelina alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 wakati Rais aliyemtangulia alipoondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi, hata hivyo hakushiriki uchaguzi wa mwaka 2013 kutokana na shinikizo la kimataifa.

Rajoelina aliingia kwenye kinyang’anyiro cha urais 2018 ambapo alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi huo, na tangu wakati huo amekuwa madarakani katika taifa hilo ambalo linatajawa kama moja kati ya nchi maskini zaidi duniani licha ya kuwa na utajiri wa maliasili.

Takribani asilimia 80 ya idadi jumla ya watu milioni 28 nchini humo wanaishi chini ya dola 2 kwa siku.