Makaburi 27 yagundulika waumini walioagizwa kufunga hadi kufa

Sehemu ya makaburi yaliyobainika kuzikwa miili ya watu 27 waliopoteza maisha kwa kufunga nchini Kenya.

Muktasari:

  • Jeshi la polisi nchini Kenya wiki iliyopita lilifanya msako mkali na kubaini watu waliokufa wakifanya maombi mfululizo kwa kufuata maagizo ya mchungaji wao.

Dar es Salaam. Polisi wa upelelezi nchini Kenya wamegundua eneo ambalo wamezikwa waumini 27 wa Kanisa la Good News International linaloongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie baada ya kutekeleza agizo la kiongozi wao la kufunga hadi kufa ili waweze kwenda kuurithi ufalme mbinguni.

Polisi walifika eneo hilo kuwaokoa washirika wa kanisa la Good News International chini ya mhubiri Paul Mackenzie na sasa wamepata makaburi zaidi.

Hivi karibuni polisi walifanya upekuzi kwenye nyumba moja eneo Shakahola Kaunti ya Malindi, ambayo iliyokuwa ikitumika kutekeleza agizo la Mchungaji Mackenzie.

Takribani watu 16 walipatikajana wakiwa kwenye hali mbaya kiafya kutokana na kufunga mfululizo bila kula chochote.

Baada ya kufika eneo hilo, waliwaokoa watu hao na kuwawahisha hospitali kwa ajili ya matibabu, huku wanne miongoni mwao wakifariki duniania.

Maofisa hao wa polisi wamepata makaburi zaidi katika msitu eneo la Kilifi ambapo washirika walitumia kufunga na kuomba.

Ripoti inasema kuwa jumla ya makaburi 27 yameweza kutambuliwa na maswali kuzuka kuhusu watu waliofariki dunia kufikia sasa.

Inaelezwa kwamba taarifa za zaidi zimefichuliwa baada manusuara kutoa ushirikiano  kwa Jeshio la Polisi nchini humo.

Mmoja wa mashududa amebainisha kwamba maombi hayo ya kufunga hadi kufa yalikuwa yakifanywa kwenye msitu mmoja eneo la Kilifi.