Marekani yawabana maofisa wa Hon Kong

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken

Muktasari:

Marekani imetangaza kuchukua hatua ya kuweka vizuizi vya visa kwa maaofisa wa Hong Kong wanaohusika kukandamiza haki nchini China.

Dar es Salaam. Marekani imetangaza kuchukua hatua ya kuweka vizuizi vya visa kwa maaofisa wa Hong Kong wanaohusika kukandamiza haki nchini China.

Hatua hiyo ya Marekani iliyotangazwa jana Ijumaa, machi 29, 2024 kufuatia kuanza kwa utekelezaji wa sheria mpya ya usalama wa taifa, Shirika la Habari la Ufaransa AFP limeripoti leo Jumamosi Machi 30, 2024.

AFP ilimnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye kwenye taarifa yake amesema: ”Beijing inaendelea kuchukua hatua dhidi ya Hong Kong  juu ya uhuru ulioahidiwa na taasisi za kidemokrasia kwa miaka iliyopita,”

Blinken amesema ukandamizaji unaoendelea, umechangiwa na "Kifungu cha 23," ya sheria ya usalama wa Taifa inayozungumzia masuala ya uhaini, uasi, ujasusi na wizi wa siri za Serikali.

Amesema: "Kuongezeka kwa ukandamizaji na vizuizi kwa mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na watu wanaopingana na Serikali wamelazimika kuchukua hatua ya kuweka vizuizi vya visa kwa maofisa wengi wa Hong Kong.

Hatua hizo zimetangazwa Blinken ambaye hakuweka wazi maofisa wanaolengwa na msimamo huo wa Marekani.

Blinken alitoa tangazo hilo baada ya Marekani kufanya mapitio ya uhuru wa Hong kong iliyoahidiwa na Beijing wakati Uingereza ilipoikavidhi mji huo mwaka 1997.

Awali, Washington iliweka vizuizi vya viza na vikwazo kwa maofisa wa Hong Kong waliotuhumiwa kukandamiza haki na uhuru ambao unatofautisha jiji hilo na China.

Hata hivyo, Serikali ya Hong kong imepinga ripoti hiyo ya Marekani ikisema, vikwazo na vizuizi vya visa vina mrengo usiosahihi wa kisiasa wa kuwatisha maofisa usalam wanaolinda Taifa.

Hon Kong imesema jiji hilo lina uhuru na sheria mpya inalinda haki za msingi na uhuru wa watu.

Mwakilishi wa wizara ya mambo ya nje ya China Hong Kong amelaani vikali hatua hiyo ya Marekani akisema huko ni kuingilia mambo ya ndani ya China.

Beijing iliweka sheria kali ya usalama wa kitaifa kwa Hong Kong mwaka 2020 ili kukomesha maandamano.

Kifungu cha 23, ambacho kilianza kutekelezwa wiki iliyopita  ni sheria ya ziada ya usalama wa kitaifa ambayo maofisa walisema ilihitajika kuziba mianya ya usalama.

Jana kituo cha habari kinachofadhiliwa na Serikali ya Marekani cha Radio Free Asia kiliripoti kufunga ofisi yake Hong Kong baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo mpya, ikitaja kuhofia usalama wa wafanyakazi wake.