Trump ajitosa mgogoro Hong Kong
Muktasari:
Mapema leo asubuhi vikozi vya Jeshi la China vikiwa na magari ya kivita yalionekana katika mji wa Hong Kong ili kuwadhibiti waandamanaji.
Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ameitaka China kutumia njia za kiutu kusuluhisha mgogoro wa waandamanaji wanaotaka demokrasia mjini Hong Kong.
Kauli hiyo ya Trump imekuja muda mchache baada ya Serikali ya China bara kuingilia kati mzozo huo kwa kupeleka magari ya kivita pamoja na wanajeshi ili kudhibiti maandamano hayo.
Picha zilizochukuliwa na Shirika la habari la AFP zilionesha maelfu ya wanajeshi wa China wakipeperusha bendera nyekundu wakiwa katika uwanja wa mchezo mjini Shenzhen mpakani mwa mji wa Hong Kong.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, Rais huyo wa Marekani alipendekeza kukutana na kiongozi wa China, Xi Jinping ili kujadili mzozo wa kisiasa ulioko Hong Kong.
Rais Trump alisema endapo maandamano hayo yatashindwa kudhibitiwa yataathiri mpango wa kibiashara baina ya mataifa hayo mawili.
Maoni ya Trump yamekuja wiki kadhaa baada ya maandamano makubwa ya wananchi wanaodai uwapo demokrasia katika visiwa vya Hong Kong.
Awali waandamanaji hao walikuwa wakipinga mswada uliokuwa ukiruhusu watuhumiwa kustakiwa kwa sheria za China bara. Hata hivyo, Serikali visiwani humo iliamua kufuta mswada huo.
Jumatano jioni, polisi waliwatawanya mamia ya waandamanaji waliokusanyika katika kitongoji cha Sham Shui Po.