Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashirika ya ndege Ulaya yasitisha safari za Iran, Iraq na Lebanon, hofu ya vita yarejea

Muktasari:

  • Mashirika ya ndege ya Ulaya yameendelea kupewa tahadhari ya kuepuka anga la Iran, Iraq na Lebanon hadi mwisho wa Agosti baada ya kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati, huku usitishaji mapigano ukielezwa kuwa bado dhaifu.

Dar es Salaam. Mashirika ya ndege ya Ulaya yameendelea kusitisha au kubadili njia za safari zake katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati baada ya mamlaka ya usalama wa anga kuongeza tahadhari kutokana na hatari ya mashambulizi mapya kati ya Marekani na Iran.

Uamuzi huo umetolewa na Wakala wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA), ambao umeelekeza waendeshaji wa ndege kuepuka kutumia anga la Iran, Iraq na Lebanon hadi Agosti 31, 2026.

Katika taarifa yake ya Jumatano Julai 8, 2026, EASA imeeleza hatua hiyo imechukuliwa kutokana na hali ya usalama kutetereka tena baada ya mashambulizi kuendelea katika ukanda huo, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, tathmini yake imehofia uwezekano wa kuendelea kwa mashambulizi ya kijeshi endapo makubaliano yaliyopo yataanguka.

Mvutano huo umeendelea baada ya Iran na Marekani kushambuliana katika siku za karibuni, hatua iliyoongeza hofu kwa sekta ya usafiri wa anga kutokana na uwepo wa maeneo yenye hatari karibu na njia muhimu za ndege.

Awali, mashirika mbalimbali ya ndege ya Ulaya yalianza kusitisha safari kwenda baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati mwishoni mwa Februari 2026 baada ya kuongezeka kwa mapigano katika eneo hilo.

Tangu wakati huo, baadhi ya safari zimekuwa zikisitishwa kwa muda au kubadilishwa njia kulingana na tathmini za kiusalama.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni Iran na Lebanon, ambako mashirika ya ndege yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya kuamua kurejesha huduma kutokana na hofu ya kuzuka tena kwa mapigano.

Hata hivyo, EASA imeondoa tahadhari ya awali iliyohusisha baadhi ya nchi nyingine za Mashariki ya Kati ikiwamo Bahrain, Kuwait, Israel, Jordan, Qatar, Oman, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, ingawa haijatoa hakikisho kamili kuwa hatari imekwisha katika maeneo hayo.

Hatua hiyo imekuja wakati Iran ikiripotiwa kuendelea kuchukua hatua za kijeshi baada ya mashambulizi yaliyolenga maeneo yanayohusishwa na Marekani katika eneo la Ghuba.

Kurejea kwa mashambulizi mivutano hiyo, tayari kumehusishwa na mitikisiko wa gharama za mafuta katika soko la dunia, ambapo bei ya mafuta ghafi iliyokuwa imeshuka hadi takribani Sh203,000 kwa pipa baada ya hali ya usalama kuimarika katika Mlango wa Hormuz. Imepanda hadi karibu Sh214,000 kwa pipa.

Hilo ni ongezeko la takribani asilimia 5.4, likionyesha jinsi mivutano katika Hormuz, ambako hupita karibu asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani, inavyoathiri haraka soko la nishati na matarajio ya mfumuko wa bei duniani

Hayo yanajiri ambapo Rais wa Marekani, Donald Trump, amekuwa akitoa kauli kwamba nchi yake inaweza kufikia makubaliano na Iran au kuendelea na hatua za kijeshi ikiwa mazungumzo yatashindikana.

Kwa upande wa Iran, viongozi wake wameendelea kusisitiza kuwa nchi hiyo ina haki ya kujilinda dhidi ya mashinikizo na mashambulizi kutoka nje.

Kwa wasafiri na kampuni za ndege, hali hiyo inahofiwa kuongeza gharama za uendeshaji kutokana na baadhi ya ndege kulazimika kutumia njia ndefu za safari kufika maeneo mbalimbali ili kukwepa maeneo yenye hatari.