Mazungumzo yataepusha machafuko Venezuela

Wiki iliyopita tuliona sehemu ya kwanza ya jinsi shinikizo la Marekani la kumwondoa Rais Nicholaus Maduro linavyohusishwa na mafuta ya Venezuela.

Leo tunaendelea kutazama jinsi vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani vinavyoiumiza nchi hiyo. Ni kutokana na vikwazo hivyo, mfumuko wa bei umefikia asilimia 950 katika mwaka huu kutoka asilimia 19 mwaka 2017.

Mshahara wa mwezi wa mfanyakazi wa kima cha chini hautoshi kununua trei ya mayai, sembuse kumtosha mtu na familia kwa wiki moja. Hali ya maisha ni ngumu sana.

Hali kama hii na ukosefu wa huduma za kijamii ilitengenezwa na mabeberu dhidi ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na hatimaye ameondolewa madarakani na jeshi na kuwekwa swahiba wake wa siku nyingi, Emmerson Mnangagwa.

Baa la njaa linaloikabili Venezuela limetengenezwa kimkakati na Marekani na washirika wake kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi. Vikwazo vinaizuia serikali ya Rais Maduro kuchukua dhahabu ya Venezuela yenye thamani ya dola 1.5 bilioni iliyoko Uingereza na pesa zilizoko kwenye mabenki ya Marekani ili izitumie kununua chakula.

Kwa nini wanakataa kuipa Venezuela dhahabu na pesa zake? Marekani imezuia mali za Venezuela zenye thamani ya dola bilioni saba.

Bila shaka mabeberu wana lao jambo kwa kuizuia serikali ya Venezuela kuchukua pesa zake halali ilizochuma kwa kuuza mafuta.

Tangu mwaka huu uanze, Venezuela imepoteza mapato na fursa za kuuza mafuta yenye thamani ya Dola 11 bilioni kwa sababu ya vikwazo vya uchumi.

Sasa tunayashuhudia matokeo ya kazi za vikwazo vya kiuchumi, siasa za mafuta na za kijiografia, kwani baadhi ya wananchi wa Venezuela wameigeuka serikali na wengine wanakimbia nchi.

Nchi yeyote duniani inakuwa haitawaliki kwa amani kama njaa inawazonga wananchi. Unaweza kutawala kwa njia moja tu – mabavu ya Jeshi. Madhara yake ni makubwa. Watu hupoteza maisha.

Njaa ilisababisha kuanguka kwa Russia ya Soviet Union. Na kama si uhakika wa chakula pamoja na kuwa makini katika ulinzi. Cuba ingeshaanguka vibaya tangu mwaka 1960 ilipowekewa vikwazo vya uchumi na Marekani. Baadhi ya vikwazo hivyo bado vipo. Rais Donald Trump anataka kuvirejesha vyote vilivyolegezwa au kuondolewa na Rais Barack Obama.

Tukumbuke kuwa Rais Trump anakabiliwa na kizungumkuti cha Russia kumsaidia kuingia White House. Hivyo, anatumia kila fursa katika uwanja kimataifa hata ndani ya Marekani kujenga ajenda ya kupindisha mwelekeo wa maoni, fikra na mitizamo ya Wamarekani ili aonekane ni kiongozi bora mwenye uwezo wa kulinda maslahi yao zaidi ya Rais yeyote.

Pia, anataka kuonyesha kwamba si kibaraka wa Rais Vladimir Putin wa Russia. Kwa sababu ya tabia zake za ubinafsi, kujisifu na kupenda kusifiwa za Rais Trump, basi anafanya kila aliwezalo kwa kutumia mabavu ya Marekani kujinyakulia umaarufu kupitia kumpindua Rais Maduro.

Januari 23 mwaka huu, Rais Trump alisema β€œAll options are on the table.”. Hii ina maana Marekani iko tayari kutumia njia zozote, hata nguvu za kijeshi, kumuondoa Rais Maduro.

Kauli hii ni ya kutaka kumwaga petroli kwenye moto. Ni fitna. Ni chachu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya Venezuela. Mola awanusuru.

Mabeberu wanataka uitishwe uchaguzi wa Rais ndani ya wiki moja huko Venezuela. Mbona hatukusia lolote kutoka kwao pale Lula Da Silva alipozuiliwa na mahakama kugombea urais wa Brazil mwaka jana ilhali sheria za uchaguzi zinampa haki hiyo?

Lengo la mabeberu ni kuivunja itikadi ya kijamaa katika Brazil pia. Wamefanikiwa. Brazil sasa inaongozwa na mhafidhina Rais Jair Bolsonaro mwenye siasa kali za mlengo wa kulia.

Lakini mbona mabeberu hawahoji demokrasia ya Marekani yenyewe. Trump hana ridhaa ya Wamarekani walio wengi. Hillary Clinton alimshinda Trump kwa kura zaidi milioni moja na nusu. Lakini Trump alishinda kwa kura za uwakilishi. Mbona mabeberu hawahoji demokrasia na maandamano ya Ufaransa? Kwa nini hawasemi Rais Macron aachie ngazi? Unafiki.

Nini kifanyike

Jibu ni kupatikana chakula, huduma za kijamii na mazungumzo.

Suala la awali la kufanyiwa kazi na washirika wa Rais Maduro ni kuisaidia Venezuela kurejesha hali ya uhakika wa chakula na huduma za kijamii kwa wananchi.

Pili hakuna lisilozungumzika. Mazungumzo yanayojumuisha pande mbili zinazohasimia pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa yatatoa dawa ya mgogoro huu unaogusa maslahi ya Russia na China na washirika wao kwa upande mmoja na Marekani na washirika wake kwa upande wa mwingine.

Umuhimu wa mazungumzo katika kutatua migogoro ni mkubwa. Mazungumzo ndiyo yalimaliza vita vya kwanza ya dunia na vita vya pili. Si mtutu wa bunduki.

Ni mazungumzo yaliyosimamisha vita vya Korea. Ni mazungumzo tu ndiyo yalimaliza mgogoro kati ya MPLA na Unita huko Angola. Angola sasa ni shwari na inastawi na kunawiri. Ni mazungumzo tu ndiyo yalimaliza mgogoro wa silaha za nyuklia huko Cuba kati ya Marekani na Russia.

Hekima na subira itawale katika kutafuta na kupatika kwa suluhisho la kudumu la mgogoro huu kwa njia ya mazungumzo ya amani.