Mfalme wa Uingereza ajutia biashara ya utumwa

Mfalme Charles III wa Uingereza na mkewe, Camilla na mgeni wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Muktasari:

Mfalme Charles III wa Uingereza ameendelea kujutia makosa yaliyofanywa na wakoloni wa nchi yake wakati wa biashara ya utumwa.

London. Mfalme Charles III wa Uingereza ameendelea kujutia makosa yaliyofanywa na wakoloni wa nchi yake wakati wa biashara ya utumwa.
Mfalme Charles alisema hayo juzi, kwenye dhifa ya kitaifa aliyomuandalia Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini aliyeko nchini humo kwa ziara rasmi ya kitaifa.

Rais Ramaphosa ndiye kiongozi wa kwanza duniani kufanya ziara rasmi ya kitaifa katika ufalme wa Mfalme Charles, aliyechukua mamlaka hayo kutoka kwa mama yake, Malkia Elizabeth aliyefariki dunia Septemba 8, 2022.

Akihutubia kwa mara kwanza kwenye dhifa ya kitaifa, Mfalme Charles alisema ufalme wake utakabiliana na alama za kikoloni.

Mfalme Charles III akihutubia kwa mara ya kwanza kwenye dhifa ya kitaifa tangu ashike uongozi huo takriban miezi miwili iliyopita, alisema ufalme wake ni kuzifanya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuwa pamoja na kuyafanya mamlaka hayo kuwa sehemu nzuri.

Mwaka jana Charles alipokuwa mwanamfalme (prince) alishutumu vitendo vya ukatili wa kutisha wakati wa biashara ya utumwa kwamba vimetia doa historia.

Hata hivyo, mapema mwaka huu alielezea huzuni yake kuhusu Uingereza ilivyohusika na biashara ya utumwa, akiwaleza viongozi wa Jumuiya ya Madola namna anavyohuzunishwa na vitendo vya kikatili vya biashara ya utumwa.
Kwenye ziara hiyo, Rais Ramaphosa alipewa heshima kwa kupokewa wanajeshi zaidi ya 1,000, farasi 230, ‘brass band’ za jeshi saba na magari ya kifalme mawili.

Tangu amekuwa Mfalme wa Uingereza baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II kilichotokea Septemba 8, 2022 na Charles kurithi mikoba ya kifalme, Rais Ramaphosa ndiye amekuwa kiongozi wa kwanza kufanya ziara rasmi ya kitaifa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Ramaphosa alikuwa afanye ziara hiyo kabla ya kifo cha Malkia Elizabeth II.

Viongozi wa Afrika Kusini waliowahi kufanya ziara rasmi ya kitaifa wakati wa Malkia Elizabeth II ni Nelson Mandela, Thabo Mbeki na Jacob Zuma.

Kwenye dhifa hiyo iliyoshirikisha watu 163, familia ya kifalme ilishiriki, wakiwamo viongozi wa Serikali. Rais Ramaphosa alifanya ziara rasmi ya kitaifa ya siku mbili nchini Uingereza.


Ahutubia Bunge

Rais Ramaphosa juzi amekuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika Kusini kuhutubia wabunge wa mabunge mawili ya Uingereza, tangu Nelson Mandela aliyepata fursa hiyo mwaka 1996.

Akihutubia bunge hilo, aliomba kuongezeka kwa uwekezaji na biashara, ikiwamo kusaidia nchi hiyo kupambana na ukataji wa umeme.

Rais Ramaphosa alisema mabadiliko ya kiuchumi na uwepo wa soko la nishati kunatoa fursa ya uwekezaji kwa wawekezaji wa kigeni, hasa kwenye eneo la upungufu wa nishati.

Pia, kiongozi huyo aliwaomba wabunge kuongeza ushirikiano kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo, kama ilivyofanyika wakati wa janga la Uviko-19.