Miamba itakavyoshindana uchaguzi Afrika Kusini

Rais wa sasa Cyril Ramaphosa (71) anayetetea kiti chake kupitia chama cha ANC.

Muktasari:

 Katika uchaguzi huo, wananchi wa Afrika Kusini watapiga kura katika uchaguzi wa kitaifa na wa majimbo ili kuchagua bunge jipya la kitaifa na mabunge ya majimbo. Bunge la kitaifa ndilo litakalomchagua rais kwa miaka mitano ijayo.

Mei 29, 2024 wananchi wa Afrika Kusini watapiga kura katika uchaguzi mkuu wa saba wa kidemokrasia wa nchi hiyo, tangu ubaguzi wa rangi ulipoisha mwaka wa 1994.

Ni uchaguzi unaotarajiwa kuwa mgumu kwa chama tawala cha African National Congress (ANC) ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 30, huku kikiwa hatarini kukosa asilimia 50 ya kura ili kujihakikishia ushindi wake.

Katika uchaguzi huo, wananchi wa Afrika Kusini watapiga kura katika uchaguzi wa kitaifa na wa majimbo ili kuchagua bunge jipya la kitaifa na mabunge ya majimbo. Bunge la kitaifa ndilo litakalomchagua rais kwa miaka mitano ijayo.

Miamba

Katika uchaguzi huo, ANC inawakilishwa na Rais wa sasa Cyril Ramaphosa (71). Kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanywa na kituo cha televisheni cha eNCA, uungwaji mkono kwa ANC uko karibu asilimia 43.4, ikiwa ni ongezeko la alama mbili kutoka miezi miwili iliyopita.

ANC inatarajiwa kushinda kwa wingi katika majimbo saba kati ya tisa ya Afrika Kusini. Hata hivyo, inakadiriwa kushindwa na chama cha Jacob Zuma cha UMkhonto we Sizwe (MK) katika jimbo lake la nyumbani la KwaZulu-Natal (KZN) na pia katika Western Cape, ambako DA inatarajiwa kushinda tena.

Kwa chama cha DA, John Steenhuisen (48) anashika nafasi ya pili kwa karibu asilimia 18.6, kikiwa na kampeni ya "kuokoa Afrika Kusini".

Democratic Alliance (DA) kwa sasa kina wingi katika jimbo la Western Cape la Afrika Kusini, likiwa na Cape Town kama mji mkuu wake. Katika uchaguzi wa 2019, kilishinda asilimia 55.45 ya kura katika jimbo hilo.

Chama cha tatu ni uMkhonto we Sizwe (Mkuki wa Taifa) - MK kinachoongozwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma (82), ambacho kwa sasa kinaungwa mkono kwa asilimia 14.1.

Chama hiki kilichochukua jina la kitengo cha zamani cha kijeshi cha ANC kilianzishwa mwaka 2023 na kinatarajiwa kupata viti kutoka ANC.


Jacob Zuma, kiongozi wa chama cha uMkhonto we Sizwe, alichokiasisi.

Licha ya Mahakama ya Kikatiba ya Afrika Kusini kumzuia Zuma kugombea ubunge Mei 20, 2024, kufuatia hukumu yake ya dharau kwa mahakama mwaka 2021; bado anabakia kuwa uso wa chama hicho na anatarajiwa kuwasilisha mgombea kutoka chama hicho kama mwakilishi wake.

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema (43) kinashika nafasi ya nne kwa kuungwa mkono kikiwa na asilimia 11.4


Julius Malema, kiongozi wa chama cha  Economic Freedom Fighters (EFF).

Hapo awali Malema alikuwa mshirika wa Zuma, lakini alifukuzwa ANC mwaka 2012 baada ya uhusiano wao kuvurugika. Ndipo akaanzisha EFF mwaka 2013.

Rais wa Afrika Kusini huchaguliwaje?

Wananchi huwa hawampigii kura moja kwa moja rais. Badala yake, wanachagua wabunge 400 wa bunge la kitaifa, ambao nao humchagua rais kwa wingi wa kura.

Iwapo ANC itapata zaidi ya asilimia 50 ya viti, Rais Cyril Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 71, huenda akachaguliwa tena kuwa rais kuhudumu muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa ANC inayotawala, ambayo iko kwenye karibu asilimia 40, huenda ikapoteza wingi wa kura zake.

Iwapo hili litatokea, basi ANC italazimika kujaribu kufanya makubaliano na vyama vingine ili kuunda serikali ya mseto na chaguo la mshirika wa mseto litategemea umbali wao kutoka alama ya asilimia 50.

Hata hivyo, isipokuwa ANC ifanye vibaya zaidi ya matarajio, kuna uwezekano mdogo wa wao kuondolewa kabisa kutoka serikalini.

Idadi ya wapiga kura

Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC), wananchi milioni 27.79 wenye umri wa miaka 18 na zaidi wamejiandikisha kwa uchaguzi wa mwaka huu, kutoka milioni 26.74 mwaka 2019.

Wapiga kura waliosajiliwa wanaoishi nje ya nchi walipiga kura zao mnamo Mei 17 na 18 na wapiga kura wenye mahitaji maalum, ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu, watapiga kura zao siku mbili kabla ya siku ya uchaguzi mnamo Mei 27 na 28.

Kwa mara ya kwanza, wagombea huru watashindana katika uchaguzi. Ili kuendana na mabadiliko haya, wapiga kura watapokea karatasi tatu za kupigia kura badala ya mbili, kila moja ikihitaji chaguo la chama kimoja au mgombea mmoja.

Katika uchaguzi wa mwisho wa kitaifa uliofanyika Jumatano, Mei 8, 2019, matokeo ya mwisho yalitangazwa siku tatu baadaye, Jumamosi, Mei 11.

Hata hivyo, mwaka huu, kwa kuwa na karatasi moja zaidi ya kuhesabu, kuthibitisha matokeo yanaweza kuchukua muda mrefu zaidi. IEC inasema itatangaza matokeo ya uchaguzi Jumapili, Juni 2, 2024.

Mwenendo wa ANC

Huu utakuwa uchaguzi mkuu wa saba wa kidemokrasia wa nchi hiyo tangu ubaguzi wa rangi ulipoisha mwaka wa 1994 wakati Nelson Mandela alipochaguliwa kuwa rais na ANC kushinda asilimia 62.5 ya viti 400 katika bunge la kitaifa na asilimia 66.36 ya kura, ambapo idadi kubwa ya wapiga kura ilikuwa asilimia 86 na asilimia 89.