Ndege yaanguka kwenye makazi, watu kadhaa wamefariki
Muktasari:
- Ndege ndogo imeanguka kwenye eneo la makazi kusini mashariki mwa Jimbo la Florida nchini Marekani na kuua watu kadhaa
Miami, Marekani/AFP. Ndege ndogo imeanguka kwenye eneo la makazi kusini mashariki mwa Jimbo la Florida nchini Marekani na kuua watu kadhaa, mamlaka za eneo zimesema.
"Ninaweza kuthibitisha kwamba tuna vifo kadhaa kutoka kwenye ndege na ndani ya nyumba zinazohamishika," Scott Ehlers, mkuu wa Zimamoto katika mji wa Clearwater, aliwaeleza waandishi wa habari jana Alhamisi Februari 1, 2024.
Ajali hiyo ilitokea jana usiku, muda mfupi baada ya uwanja wa ndege ulio karibu kupokea taarifa kuhusu ndege hiyo kupata hitilafu, Ehlers alisema.
Maofisa Zimamoto walifanikiwa kuuzima moto huo uliosababishwa na ndege iliyoanguka.
Angalau nyumba tatu ziliharibiwa na moto na ya nne ilianguki moja kwa moja na ndege, kwa mujibu wa mkuu wa Zimamoto.
Wakazi wa nyumba zingine hawakujeruhiwa, aliongeza.
Rubani wa ndege hiyo, yenye injini moja, Beechcraft Bonanza V35, alikuwa ameripoti hitilafu ya injini kabla ya ajali kutokea, vyombo vya habari vya ndani viliripoti vikinukuu Mamlaka ya Anga.