Ndege yageuza ikiwa angani kuelekea Uingereza

Muktasari:

  • Hii ilikuwa ni muda mfupi kabla ya nchi hiyo kupiga marufuku ndege aina ya Boeing 737 MAX 8 kutua Uingereza

Instanbul, Uturuki. Ndege mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 za Shirika la Ndege la Uturuki ambazo zilikuwa zikisafiri kuelekea Uingereza zimelazimika kugeuza zikiwa angani baada ya Uingereza kuzipiga marufuku kutua katika viwanja vya Uingereza.

Ndege hizo zilikuwa zimeanza safari katika Uwanja wa Kimataifa wa Instanbul, Uturuki, kabla ya Mamlaka ya Kusimamia Safari za Anga Uingereza kutangaza marufuku hiyo.

Na kufuatia hatua hiyo, takriban watu 300 waliokuwa wamepanga kusafiri kutoka Uingereza kwenda jijini Instanbul walikosa usafiri wakiwa katika viwanja vya ndege vya Birmingham na Gatwick.

Hatua hii imechukuliwa na Uingereza baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ya aina hiyo kuanguka na kuua watu 157  Jumapili dakika sita baada ya kuruka.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi.

Mpaka sasa zaidi ya mataifa 13 yamepiga marufuku ndege hizo zinazotengenezwa Marekani.

Miongoni mwa mataifa hayo ni China, Australia, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ireland, Ufaransa, Indonesia, Brazil, Afrika Kusini, Mexico, Ujerumani na Ethiopia.