Njia ya kuelekea kumpindua Moi-4

Rais Daniel arap Moi akiwa katika moja ya mikutano ya siasa

Muktasari:

  • Katika toleo la jana tuliona jinsi utawala wa miaka minne ya Rais Daniel arap Moi ulivyokabiliwa na maandamano ya wanafunzi na wapinzani wa kisiasa dhidi yake ndani na nje ya Bunge.

Katika toleo la jana tuliona jinsi utawala wa miaka minne ya Rais Daniel arap Moi ulivyokabiliwa na maandamano ya wanafunzi na wapinzani wa kisiasa dhidi yake ndani na nje ya Bunge


Chuo Kikuu cha Nairobi kiliongoza katika maandamano ya mara kwa mara kiasi kwamba hata baadhi ya wanafunzi walifukuzwa na wahadhiri, akiwamo Ngugi wa Thiong’o, kushughulikiwa.

Rais Moi alipata upinzani bungeni. Wabunge walioonekana kuwa na msimamo dhidi ya Serikali walikabiliwa na wakati mgumu na wengine kama mbunge wa Nyeri, Waruru Kanja alifungwa gerezani.

Mmoja wa wanasiasa waliosikitishwa na matukio hayo ni aliyekuwa Makamu wa Rais, Jaramogi Oginga Odinga ambaye wakati huu alikuwa ameanza kuwa adui wa kisiasa wa Rais Moi.

Kufikia mwanzoni mwa mwaka 1982, Odinga hakuweza kuvumilia tena. Katika mkutano na waandishi wa habari aliikosoa waziwazi Serikali ya Moi. Alisema uchumi umedorora, ukosefu wa ajira unaongezeka na ufisadi.

Alidai kuwa hali mbaya ya uchumi ilisababishwa na ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za kigeni, uingizaji wa bidhaa za anasa, mipango mibovu, utegemezi kupita kiasi na matumizi mabaya ya misaada kutoka kwa wafadhili.

Katika orodha ya malalamiko, Odinga aliukosoa uhusiano wa karibu wa kijeshi kati ya Kenya na Marekani uliobuniwa na Serikali ya Moi. Pia alikuwa na wasiwasi kuhusu uwiano kati ya sera ya kiuchumi ya Kenya na itikadi changa ya uliberali mamboleo iliyoanzishwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia huko Washington.

Moi aliweka wazi kuwa hatavumilia kashfa zaidi zinazotolewa na Odinga au wafuasi wake na akasema hadharani wazo lake la kurejesha sheria ya kuwaweka watu kizuizini bila kufunguliwa mashtaka. Alikaririwa na jarida ‘Weekly Review’ la Aprili 23, 1982 akisema: “Labda wakati umefika wa kuamua kuchukua hatua hii.”

Odinga hakumsikiliza Moi tena kwa sababu aliona kuwa ukimya wake katika miaka minne ya mwanzo ya utawala wake haukumletea thawabu yoyote.

Alitumia ziara ya Mei 1982 jijini London, Uingereza, kuhutubia Chama cha Labour ambako aliukosoa vikali utawala wa Moi na alipendekeza kuwa chama kingine cha kisiasa kilikuwa muhimu kuanzishwa nchini Kenya.

Alisema: “Mifumo hii ya chama kimoja inakuwa mifumo isiyo ya chama. Marais wanajidai wenyewe kujipa nafasi ya kuwa watunga sheria na wasimamizi wa sheria. Wanatawala kwa amri na kauli zao wenyewe. Wanajiundia vikundi vya watu kuwaunga mkono na kuunyonya umma.”

Wakati Odinga akitoa madai hayo mjini London, mjini Nairobi mwanasiasa mwingine mpinzani wa Moi, George Anyona alipokea ujumbe huo na akasema chama kingine cha siasa ni cha lazima kwa Kenya kwa sababu kulingana na alivyodai ili “kuepuka kuanguka katika dhuluma mbaya za chama kimoja ambazo zimekithiri barani Afrika leo.”

Kwa Anyona na wengine wengi ilionekana kuwa KANU imekuwa “tishio kubwa zaidi kwa demokrasia nchini Kenya.” Hizi kauli zilimtisha Rais Moi.

Sambamba na hayo, viongozi wa wanafunzi walitoa wito kwa Serikali na KANU kuheshimu katiba ya Kenya, hasa kifungu ambacho kinahakikisha haki za Wakenya kuunda au kuwa wa chama chochote cha kisiasa wapendacho, lakini Serikali ilizuia jambo hilo. Mmoja wa wanasiasa machachari wa fukuto la kuanzishwa kwa vyama vingi alikuwa Mukaru Ng’ang’a, aliionya Serikali isijaribu kuzuia kuanzishwa kwa chama kingine cha siasa, lakini Rais Moi alimpuuza.

Moi alimkashifu Odinga akisema anajihusisha na siasa za mgawanyiko na propaganda dhidi ya mawaziri wa baraza la mawaziri la Kenya zinazolenga kuwagawanya watu wa Kenya. Kwa sababu hiyo, Odinga alifukuzwa kwenye chama cha KANU. Ndoto yake ya kuanzisha chama kingine cha siasa iliyeyuka wakati Waziri wa Katiba, Charles Njonjo alipowasilisha hoja ya Bunge ya kuratibu Serikali ya chama kimoja ndani ya katiba. Hoja hiyo iliungwa mkono na Kenya ikawa nchi ya chama kimoja.

Zaidi ya wiki moja mwishoni mwa Mei na mapema Juni 1982, wapinzani wa Rais Moi ambao ni George Anyona, Mwangi Stephen Muriithi na John Khaminwa walitiwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka. Awali Muriithi ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa idara ya upelelezi, alikuwa wa kwanza kutiwa ndani. Baadhi ya wahadhiri nao waliwekwa ndani na sababu ni zile ambazo Rais Moi alidai walikuwa wakihubiri “siasa za upotoshaji na ghasia” na kuwashutumu kupanga njama za kuiangusha Serikali yake.

Kutokana na ghasia katika Chuo Kikuu cha Kenyatta Mei 1982, Dk Al Amin Mazrui, Willy Mutunga na Maina wa Kinyatti, wote wahadhiri katika taasisi hiyo, walikamatwa na chuo kikafungwa kwa muda. Haikuishia hapo, wabunge wengine nao wakatiwa kizuizini.

Kadiri idadi ya waliowekwa kizuizini ilivyoongezeka huku Serikali ikidai itazidi kuwatia wengine ndani, baadhi ya wapinzani wa muda mrefu wa Serikali walitishika na hivyo wakalazimika kuikimbia nchi. Sauti za wapinzani zilipokandamizwa zaidi, walianza kutafuta namna ya kuiondoa Serikali madarakani kwa njia za kijeshi.

Gazeti lililoitwa ‘Pambana’ lililosambazwa Nairobi Mei 1982, liliandika kuwa utawala wa Moi unashutumiwa kwa “kupanda mbegu ya mafarakano na uadui miongoni mwa watu wetu, na kupora fedha nyingi na utajiri wa Taifa.”

“Uhalifu wote huu umetekelezwa kwa jina la “maendeleo na ustawi” na migawanyiko isiyo ya kawaida badala ya ‘upendo, amani na umoja.’ Huu si uhuru ... ni ukoloni mamboleo,” lilisisitiza gazeti hilo.

Rais Moi hakujali, badala yake alisema: “Vita hivi sasa vitaendelea hadi tuisafishe nchi yetu ... Adui ni kama panya wanaotia sumu akilini mwa watu na sikuwa na njia nyingine ila kuwaweka kizuizini.”

Kufikia hatua hii, zikaanza kuwapo tetesi za kufanyika mapinduzi ya kijeshi. Vitengo vya usalama vilianza kusikia tetesi hizo, lakini zikachukuliwa kama ni uvumi wa kawaida tu kama ilivyokuwa mwaka 1971. Tetesi hizo zilianza kama uvumi ambao wengi walifikiria haukupaswa kuwa sababu ya hofu, lakini kuelekea Agosti uvumi ulizidi kuongezeka.

Kulingana na uvumi huo, mapinduzi yalikuwa yafanyike wiki ya mwisho ya Julai 1982. Ingawa huenda umma wa Wakenya ulikuwa haujausikia uvumi huo, vitengo vya usalama walikuwa wameusikia. Lakini kwa kuwa sehemu ya habari zilizosambaa zilibainika kuwa za uongo, basi na uvumi huo haukutiliwa sana maanani.

Wakati kukiwa na tetesi hizo, maandalizi ya kufanya mapinduzi yalikuwa yakiendelea. Mikutano ilikuwa inafanywa na baadhi ya wanajeshi wa vyeo vya chini. Je, uvumi uligeukaje kuwa hali halisi?

Tukutane toleo lijalo.