Rais Moi na vuguvugu la kisiasa na wananchi-3

Daniel Arap Moi

Muktasari:

  • Huko Kenya Agosti 1, 1982 kulifanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoongozwa na mwanajeshi wa cheo cha chini, Hezekiah Ochuka aliyedumu kama Rais wa nchi hiyo kwa takribani saa sita tu.

Huko Kenya Agosti 1, 1982 kulifanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoongozwa na mwanajeshi wa cheo cha chini, Hezekiah Ochuka aliyedumu kama Rais wa nchi hiyo kwa takribani saa sita tu.

Ingawa ilionekana jaribio hilo lilipangwa kwa muda mfupi, kulikuwa na mambo mengi yaliyochangia Wakenya kuichoka Serikali ya Rais Daniel Arap Moi, kwa kuwa mambo mengi yalikuwa yametendeka kwa miaka kadhaa kabla ya siku ya tukio hilo.

Wakosoaji wa Serikali ya Mzee Jomo Kenyatta, aliyefariki dunia Agosti 22, 1978 na kumwachia Moi kijiti cha urais, walichochea vita mpya dhidi ya Serikali. Vita hiyo ilishika kasi kutokana na kasoro za wazi zilizoonekana katika utawala wa Rais wa pili wa Kenya.

Sera za Serikali katika nyanja mbalimbali zilisababisha wasiwasi mkubwa kwa Wakenya, Moi alidumisha uhusiano wa karibu na mataifa ya magharibi ulioanzishwa na Kenyatta.

Makubaliano yaliyofikiwa na Marekani yaliiruhusu kujipenyeza kwenye vituo vya kijeshi vya Kenya huku yakithibitika kuwa na utata katika vipengele vyote vya uhusiano wa kirafiki unaofurahiwa na mataifa yenye nguvu.

“Kenya haijawekwa rehani au kuuzwa kwa wageni, wanyonyaji na wabadhirifu,” mwanasiasa wa Kenya na mpinzani wa Rais Moi, Jaramogi Oginga Odinga aliandika katika barua ya wazi kwa Bunge la Marekani mwanzoni mwa mwaka 1982.

Ukosefu wa ajira uliongezeka karibu asilimia 20 wakati deni la Taifa na mfumuko wa bei uliongezeka zaidi mwishoni mwa miaka ya 1970 na mapema miaka ya 1980.

Kwa jumla mfumuko wa bei mwaka 1978 ulikuwa asilimia 12.5 na ilipofika mwaka 1980, ukuaji wa uchumi ulikuwa ukipungua kadiri gharama ya uagizaji bidhaa kutoka nje ulivyopanda na mahitaji ya mauzo ya nje kupungua.

Na ilipofika mwaka 1981, matumizi ya Serikali yalizidi mapato kwa Dola570 milioni kwa wakati huo. Wakati Serikali ilikopa pesa ili kupunguza nakisi ya biashara iliyokuwa ikiongezeka, deni ambalo Kenya ilidaiwa ng’ambo lilifikia Dola 1 bilioni za Marekani mwaka 1980. Mkopo wa Dola 310 milioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ulikubaliwa mwaka 1981 baada ya hali kuwa ngumu.

Mambo yaliyo nje ya udhibiti wa Serikali ya Kenya yalichangia mabadiliko ya taswira ya kiuchumi. Kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ilikuwa sababu mojawapo ya matatizo ya kiuchumi na ukame wa mwaka 1979 na 1980 uliathiri sana kilimo ambacho ni sekta muhimu.

Wakati huohuo, bei za mazao ya biashara kama chai na kahawa zilishuka; zaidi ya yote, kila mwaka kulikuwa na Wakenya wengi wa kulishwa, kuelimishwa na kupatiwa huduma za matibabu.

Hadi mwanzoni mwa mwaka 1981, Wakenya wapatao 225,000 walikuwa wakiingia katika soko la ajira kila mwaka. Ingawa uchumi ulikua kwa asilimia 2.4 mwaka 1980, hii ilikuwa chini sana kuliko kiwango cha ongezeko la idadi ya watu.

Isitoshe, shilingi ya Kenya ilishushwa thamani kwa takribani asilimia 25 ya thamani yake mwaka wa 1981. Pia, jitihada zaidi zilifanywa ili kupunguza mahitaji ya uagizaji bidhaa kutoka nje.

Kwa mujibu wa jarida ‘Weekly Review’ la Desemba 5, 1980, usimamizi mbaya wa Serikali na ufisadi uliokithiri vilisababisha uhaba wa chakula na bidhaa nyingine muhimu madukani. Watu binafsi waliokuwa karibu na Rais walikuwa huru kufanya wapendavyo kufaidika na ufisadi huo.

Vyakula vya msingi vilikuwa vikisafirishwa kwa magendo kuvuka mipaka ya Kenya kwenda kuuzwa kwa bei ya juu nje ya nchi, huku Wakenya wakivikosa.

Kwa kuwa walikuwa wakiuza tena misaada ya chakula cha kibinadamu kwenye soko la kimataifa, ilifanya hali mbaya kuwa mbaya zaidi.

“Kati ya mwaka 1978 na 1981 kundi la baadhi ya mawaziri lilitumia ukaribu wao na wenye mamlaka kuuza nje akiba ya kimkakati ya mahindi na walipokuwa huko walipata haki ya kuagiza nafaka pekee,” liliandika jarida ‘Independent Kenya’, lililochapishwa London, Uingereza.

Punguzo la matumizi ya Serikali lililokubaliwa na IMF lilileta matokeo yasiyotarajiwa. Mishahara ya watumishi wengi wa Serikali ilipunguzwa, jambo lililochochea zaidi ufisadi kwa maofisa wa umma waliolazimika kutafuta njia mbadala za kujipatia kipato kilichopunguzwa.

Maandamano ya kwanza dhidi ya utawala wa Rais Moi yalianza katika Kampasi za Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kenyatta mwishoni mwa mwaka 1979.

Kwa mfano, katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kitendo cha Serikali kukataa kumrejesha Ngugi wa Thiong’o katika wadhifa wake wa kitaaluma kuliibua hasira kubwa miongoni mwa baraza la wanafunzi.

Ngugi alikuwa amekamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mwaka mmoja bila kufunguliwa mashtaka. Hii ilitokana na msimamo wake dhidi ya Serikali. Katika maandamano hayo wanafunzi kadhaa walifukuzwa.

Katika muda wa miaka mitatu iliyofuata, maandamano ya wanafunzi na kufungwa kwa vyuo lilikuwa jambo la kawaida katika kampasi kuu mbili za chuo kikuu. Machafuko hayo yalienea katika shule za msingi na sekondari pia. Wanafunzi wa shule waliingia katika wimbi la migomo kutokana na hali mbaya.

Rais Moi aliamini maandamano na migomo ya wanafunzi ilichochewa na wahadhiri wanaoipinga Serikali yake. Maandamano yaliposhika kasi, bungeni nako ziliibuka sauti zinazopingana.

Wapinzani dhidi yake walizidi kuongezeka. Machi 2, 1981, wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi walipanga kufanya maandamano yao ya kila mwaka kuadhimisha kifo cha mwanasiasa Josiah Mwangi Kariuki aliyeuawa Machi 2, 1975.

Moi aliamuru maandamano hayo yasitishwe, lakini wanafunzi walimpinga. Utawala wa chuo nao ulijaribu kuzuia maandamano hayo lakini ulishindwa.

Stanley Oloitipitip, ambaye alikuwa Waziri wa Masuala ya Ndani wa Kenya, hakuweza kuelewa ugomvi kati ya Serikali na wanafunzi ulikuwa juu ya nini, kisha akatania: “Baba yangu amekufa na kila mtu atakufa ... Sioni kwa nini wasomi wapoteze muda wao mitaani kupiga kelele kuhusu JM (Josiah Mwangi) ilhali amekufa.”

Wakati huo huo, Moi alikosana na aliyewahi kuwa makamu wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga kiasi kwamba alimzuia hata kugombea kiti cha ubunge cha Bondo.

Tahariri ya gazeti la ‘The Nation’ lilimtaka Moi kubatilisha uamuzi wa kumzuia Odinga kugombea Bondo, matokeo yake wafanyakazi watano waandamizi wa gazeti hilo walikamatwa ingawa waliachiwa baadaye.

Wanafunzi walifanya maandamano mengine yaliyogeuka vurugu baada ya kukabiliwa na polisi. Chuo Kikuu cha Nairobi kikafungwa. Wahadhiri wanaojulikana kuwa na misimamo mikali walianza kunyanyaswa. Mmoja wao ni mwanahistoria Mukaru Ng’ang’a, aliyekamatwa mara kadhaa kwa makosa madogo katikati ya mwaka 1981.

Je, yote haya ndiyo yaliyochangia maandalizi ya jaribio la mapinduzi?

Tukutane toleo lijalo.