Mtangazaji alipotakiwa kutangaza Ochuka ni Rais-2

Wanajeshi wakifanya doria katika mitaa ya Nairobi baada ya mapinduzi yaliyoshindwa mwaka 1982.

Muktasari:

  • Jana, tulisimulia jinsi Serikali ya Daniel Arap Moi wa Kenya ilipotiwa majaribuni baada ya baadhi ya wanajeshi wa vyeo vya chini kufanya jaribio la kumwondoa madarakani.

Jana, tulisimulia jinsi Serikali ya Daniel Arap Moi wa Kenya ilipotiwa majaribuni baada ya baadhi ya wanajeshi wa vyeo vya chini kufanya jaribio la kumwondoa madarakani.

Wanajeshi hao waliidhibiti Kenya kwa saa sita kabla ya kuelemewa huku wengine wakikimbilia Dar es Salaam, Tanzania.

Jaribio hilo liliongozwa na Hezekiah Rabala Ochuka aliyekuwa na miaka 29 huku akiwa na cheo cha ‘Private’ katika Jeshi la Anga la Kenya (KAF).

Ochuka aliitawala Kenya kwa takriban saa sita Jumapili ya Agosti 1, 1982 na kujiita mwenyekiti wa kundi la Baraza la Ukombozi wa Watu wa Kenya lililopanga kuchukua nafasi ya Rais Moi.

Ujuzi wa kijeshi wa Ochuka na uhusiano wake na wengine ulifanya aweze kuandaa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Serikali ya Kenya.

Ochuka hakufanikiwa katika jaribio lake la kupindua kabisa Serikali ya nchi yake, lakini aliweza kudhibiti nchi nzima ya Kenya kwa saa sita.

Ochuka aliyekuwa Mjaluo mzaliwa wa Nyakach, Wilaya ya Kisumu, alisoma Shule ya Msingi ya Naki Kabete na Sekondari ya Mirogi.

Ochuka na kaka zake watatu walililelewa na mama yao aliyekuwa akifanya kazi ngumu.

Septemba 14, 1976 aliajiriwa KAF huko Mombasa na alipitia mafunzo ya kijeshi ya wiki nane katika Kambi ya Jeshi ya Lanet mjini Nakuru kisha akapelekwa katika kambi ya ndege za kivita ya Eastleigh.

Kati ya mwaka 1976 na 1978, alipata mafunzo ya msingi ya vifaa vya umeme na baadaye akawa anafanya kazi kwenye mabanda ya kuhifadhi ndege za kijeshi.

Kuanzia Oktoba 30, 1978 hadi Januari 21, 1980, alihudhuria kozi huko RAF Cosford, Uingereza kisha akaenda kufanya kazi akiwa ‘Senior Private Grade-I’, mwenye cheo cha pili kutoka chini katika Jeshi la Kenya.

Kwa mujibu wa mwandishi Jim Bailey katika kitabu chake ‘Kenya the National Epic,’ Ochuka alitamani siku moja awe Rais wa Kenya, hata kwenye meza yake jeshini palikuwa na maneno yaliyochongwa yaliyosomeka “Rais ajaye wa Kenya.”

Ndoto yake hiyo aliilazimisha Jumapili ya Agosti 1, 1982, baada ya kufanya jaribio la mapinduzi ya kijeshi na kuitawala Kenya kwa saa sita, baada ya kuongoza kundi la wanajeshi wenzake wa vyeo vya chini.

Tukio hilo limebaki kama kumbukumbu kubwa katika historia ya Kenya kwa sababu lilikuwa ni mara ya kwanza kutokea tangu Taifa hilo lipate uhuru Desemba 12, 1963.

Zaidi ya raia 200 na wanajeshi 100 waliuawa siku hiyo na takribani maduka 1,000 yalivamiwa katika machafuko kabla wanajeshi wa kikosi cha nchi kavu walioongozwa na aliyekuwa kiongozi wao Mahmoud Mohamed.

Kiongozi huyo baadaye alikuwa mkuu wa majeshi Kenya na kurejesha utawala wa raia na kutuliza machafuko hayo.

Katika shambulio hilo Wakenya walizinduliwa na milio ya risasi na mabomu kisha wakasikia redio ya nchi hiyo, Sauti ya Kenya (VoK) ambayo sasa inajulikana kama Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), ikitangaza kuwa wanajeshi walikuwa wakipigana na askari waaminifu wa Rais Moi.

Wanajeshi hao walivamia studio za VoK baada ya kwenda nyumbani kwa mtangazaji Leonard Mambo Mbotela, kumteka na kumlazimishwa atangaze kuwa Serikali imepinduliwa.

Mbotela aliyekuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili na Lugha za Kiasili VoK, alitekwa nyumbani kwake Mtaa wa Ngara, Nairobi.

Ilikuwa ni muda mfupi umepita tangu Mbotela aliporejea nyumbani kulala baada ya kumsindikiza dada yake uwanja wa ndege aliyekuwa akisafiri kwenda Canada.

Ilipotimu saa 10:45 alfajiri, Mbotela aliamshwa na milio ya risasi nje ya nyumba yake. Alidhani ni ‘wakora’ waliokuwa wakikabiliana na maofisa wa polisi, lakini ghafla, dirisha la chumba chake cha kulala liligongwa kwa nguvu.

Alipofungua dirisha kutazama alimwona dereva wa VoK aliyeitwa Wainaina ametekwa na wanajeshi hao kutoka studio za redio hiyo.

Kwa haraka alidhani kulikuwa na tatizo la kiufundi kazini, hivyo walimfuata kumpa taarifa.

Mbotela akiwa na mavazi ya kulalia, alitoka ndani kwenda nje kuonana na Wainaina, lakini ghafla akakutana na watu waliovalia sare za jeshi huku wamebeba silaha.

Mmoja wa wanajeshi hao akamwita Mbotela kwa jina lake la kwanza, “Leonard. Wewe ndio tunayekutaka. Tunakupa dakika tatu uvae kisha twende.”

Aliyetoa amri hiyo ni Ochuka aliyekuwa ameandamana na wanajeshi kumi.

Baada ya Mbotela kuvaa akiwa chini ya mtutu wa bunduki, walimwamuru aingie kwenye gari lao aina ya ‘Land Rover’ na wakaondoka naye huku akimwacha mkewe na watoto. Hakujua kama angerejea akiwa hai au amekufa.

Kabla ya kufika studio, wanajeshi hao walipora viatu madukani katikati ya Jiji la Nairobi na wakamwambia Mbotela achukue vyake, lakini baadaye waligundua kuwa viatu vingi walivyopora vilikuwa vya mguu wa kushoto.

Walipofika kwenye studio za VoK, Ochuka alichukua karatasi na kuandika taarifa fupi. Akampa Mbotela na kumlazimisha aisome hivi: “Mimi ni Leonard Mambo Mbotela. Serikali ya Moi imepinduliwa na sasa Rais ni Jenerali Hezekiah Ochuka. Wananchi mnaombwa mkae nyumbani, wafungwa wote waachiliwe na polisi sasa ni raia.”

Ochuka na wenzake wapatao 20 waliokuwa wametanda kwenye studio, walimwamuru Mbotela arudi kuisoma taarifa hiyo mara tatu huku wao wakiwa wamesimama kando wakimshikia bunduki.

Baada ya kurudia kuisoma mara tatu, Mbotela aliwauliza kwa nini walimchagua yeye kusoma tangazo hilo? Wakamjibu ni kwa sababu alifahamika sana na kuaminika zaidi kwa raia wengi.

Pia, walimwambia raia wakisikia ametangaza yeye wataamini kuwa taarifa hiyo ni kweli.

Ni kitu gani kiliwachochea Ochuka na wenzake kufanya jaribio hilo la mapinduzi? Mipango ya mapinduzi ulikuwaje na iliandaliwa vipi na kwa muda gani?

Itaendelea kesho.