Jaribio la askari wa KAF kumpindua Rais Moi -1

Daniel Arap Moi

Muktasari:

  • Jumapili ya Agosti 1, 1982 kulifanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi Kenya ili kuipindua Serikali ya Rais Daniel Arap Moi.

Jumapili ya Agosti 1, 1982 kulifanyika jaribio la mapinduzi ya kijeshi Kenya ili kuipindua Serikali ya Rais Daniel Arap Moi.

Saa tisa alfajiri ya siku hiyo, wanajeshi wenye vyeo kutoka Jeshi la Anga la Kenya (KAF) waliteka Kambi ya Jeshi la Anga ya Eastleigh, nje kidogo ya Nairobi.

Na ilipofika saa 10 alfajiri ya siku hiyo, uwanja wa ndege za jeshi wa Embakasi karibu na Nairobi nao ukawa tayari umetekwa.

Saa 12 asubuhi mwanajeshi aliyekuwa na cheo cha pili, Hezekiah Ochuka na mwenzake Sajenti Pancras Oteyo Okumu walikiteka Kituo cha Redio cha Sauti ya Kenya (VoK) katikati mwa Nairobi.

Mtangazaji maarufu wa Sauti ya Kenya, Leonard Mambo Mbotela, alifuatwa na wanajeshi nyumbani kwake alfajiri, akatekwa na kupelekwa ofisi za redio ya Sauti ya Kenya.

Alipofikishwa huko alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kutangaza redioni kwamba, Serikali ya Moi imepinduliwa.

Akifanya kazi kwa amri ya mwanajeshi Ochuka, Koplo Bramwel Injeni Njereman alikuwa akiongoza njama ya kulipua Ikulu na makao makuu ya polisi mjini Nairobi.

Koplo Njereman aliwalazimisha marubani watatu (meja David Mutua, Kapteni John Mugwanja na Kapteni John Baraza) kurusha ndege mbili aina ya ‘F-5E Tiger’ na ‘Strikemaster’ ambazo zingetumika katika operesheni hiyo ya kulipua Ikulu na makao makuu ya polisi.

Marubani hao watatu walipokuwa nyumbani na familia zao ambao ni wanajeshi waasi katika Kituo cha Ndege cha Laikipia, ambacho wakati huo kilijulikana kama KAF (Kenya Air Force) Nanyuki, hawakujua kilichokuwa kinaendelea.

Ndege aina ya ‘F-5E Tiger’ ya Meja Mutua yenye viti viwili ilipakiwa mabomu; na ndege aina ya ‘Strikemaster’ ya Kapteni Baraza ilikuwa na roketi za kulipuka.

Marubani hao watatu walikusanywa kwa mtutu wa bunduki kutoka kwenye makazi yao.

Koplo Njereman aliwaamuru wajitokeze na kuingia kwenye vyumba vyao vya marubani. Walipewa amri kwamba lengo ni kwenda kulipua Ikulu ya Nairobi na makao makuu ya polisi Nairobi.

Koplo Njereman alikaa kiti cha nyuma kwenye ndege nyuma ya Meja Mutua kusimamia utekelezaji wa mpango huo.

Licha ya kusimamia njama za kwenda kuilipua Ikulu ya Nairobi kwa kutumia ndege ya jeshi, kabla ya hapo Koplo Njereman hakuwahi kusafiri kwa ndege, achilia mbali kuongoza njama kubwa kiasi hicho cha kuipindua Serikali na kutumia ndege kuilipua Ikulu. Kwa hiyo Mutua aliamua kumfundisha somo.

Marubani walipokuwa wakiwasiliana kwa njia ya siri, walikubali kutekeleza amri zao waasi kwa ujanja ili kumvuruga Koplo Njereman.

Ujanja huo ulifanya kazi. Marubani walitupa mabomu katika msitu wa Mlima Kenya wakijifanya wameilipua Ikulu na kurudi Kambi ya Nanyuki.

Mapinduzi hayo yalipangwa kimkakati ili yafanyike sambamba na mazoezi ya kivita yaliyokuwa yakifanyika Lodwar Kenya wakati vitengo vingi vya jeshi na viongozi wakuu walikuwa huko, mbali na Nairobi. Maofisa waandamizi waliokuwapo wakati huo ni Luteni Jenerali John Sawe (Mkuu wa Jeshi), Meja Jenerali Mahmoud Mohamed (naibu wa Sawe), Brigedia Bernard Kiilu (Mkuu wa Operesheni Makao Makuu) na Meja Humphrey Njoroge (mnadhimu aliyesimamia mafunzo katika Makao Makuu ya Jeshi).

Baadaye ilijulikana kuwa aliyekuwa kiongozi wa maasi hayo ni Hezekiah Ochuka, ambaye cheo chake cha ‘Senior Private Grade-I’ kilikuwa cha pili kutoka chini kabisa Jeshi la Kenya.

Ochuka aliitawala Kenya kwa saa sita tu, ilipofika mchana wa siku hiyo baada ya majeshi yanayomtii Rais Moi kumrejesha madarakani yakiongozwa na Meja Jenerali Mahmoud Mohamed, alilazimika kukimbilia Tanzania.

Ochuka alipoona mambo yamekorogeka, alimteka Luteni Jenerali Nick Leshan na kumlazimisha kuingia kwenye gari dogo aina ya ‘Alfasud’ pamoja na Meja William Marende aliyekuwa rubani wa ndege za kijeshi. Gari iliendeshwa hadi ilipokuwa imeegeshwa ndege aina ya ‘Buffalo 210.’

Kiti cha nyuma cha gari hilo alikuwa amekaa Sajini Pancras Oteyo Okumu aliyekuwa ameiteka Redio ya Sauti ya Kenya (VoK) alfajiri ya siku hiyo. Akiwa kwenye gari alikuwa ameshikilia bunduki aina ya SMG.

Baada ya kuingia kwenye ndege, Ochuka alimwamuru Luteni Jenerali Leshan arushe ndege kuelekea Dar es Salaam, Tanzania.

Tatizo lilikuwa Luteni Jenerali Leshan hakuwa na ramani na hakuwa na wasaidizi, hivyo ilimbidi kuirusha ndege hiyo hivyo hivyo. Ndege ya Buffalo ilihitaji angalau watu watatu ili kuirusha, yaani rubani, rubani mwenza na msoma ramani.

Luteni Jenerali Leshan aligundua rubani mwenza wake, Meja Marende hakuwa na manufaa sana kwake kwa kuwa alikuwa na uzoefu wa kurusha “ndege ndogo za mafunzo.”

Lakini kulikuwa na shida nyingine. Hawakuwa na vibali vya kuingia Tanzania, wakati wanakaribia Dar es Salaam, walibakiwa na mafuta ambayo yasingeweza kuwachukua zaidi ya dakika tano angani. Wakati ndege yao ikiwa imebakiwa na mafuta yasiyotosha kuendelea na safari kwa dakika tano zaidi, Serikali ya Tanzania iliwazuia kutua, ndipo Meja Leshan alipotangaza kuwa yuko katika hali ya dharura.

Alitoa taarifa kwa mamlaka za Tanzania kuwa, ndani ya ndege alikuwa na mtu aliyekuwa ameshika bunduku nyuma yake na kwamba ndege ilielekea kuishiwa mafuta, kwa hiyo aliomba kutua kwa dharura. Alikubaliwa.

Baada ya kutua Dar es Salaam, Ochuka aliomba hifadhi ya kisiasa na kudai alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ukombozi wa Watu wa Kenya na ndiyo maana amekimbia Kenya kama mkimbizi wa kisiasa.

Lakini mjini Nairobi, Agosti 12, 1982 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Sharad Rao aliomba hati ya kukamatwa kwa Ochuka na wenzake na kurejeshwa Kenya. Hati hiyo ilitolewa na Jaji Abdul Rauf.

Hata hivyo, Septemba 21, 1982 Mahakama ya Tanzania ilikubaliana na Ochuka na kutupilia mbali ombi la Kenya la kuwarejesha ‘wakimbizi’ hao.

Jaji Goodwill Korosso alisema ushahidi ulionyesha kuwa wanajeshi hao walikubaliana na mpango wa kukimbilia Tanzania na huenda walikubali wazo hilo baada ya kubaini maisha yao yapo hatarini kutokana na kuvamiwa na majeshi ya Serikali.

“Inawezekana wakuu hao walikubali kuja Tanzania kwa kuhofia usalama wa maisha yao upo hatarini, njia pekee ya kujiokoa kutokana na kuendeleza vikosi vya askari wa miguu kwenye kambi ya Eastleigh ilikuwa ni kutorokea Tanzania.

“Hata hivyo, wakuu wawili wa kijeshi hawakuwa na vyeo kwenye mabega yao vya kuwatofautisha na watumishi wengine,” alisema Jaji Korosso katika uamuzi wake.

Je, ni watu gani walishirikiana na Hezekiah Ochuka kufanya mapinduzi hayo? Itaendelea kesho.