Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chanjo ya mifugo kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji(kulia) akizindua chanjo ya mifugo kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani katika Kijiji cha Kikalo Kata ya Miono Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani Julai 9, 2025 ambapo shughuli ya chanjo itafanyika kwa siku 30 katika Mkoa huo. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Chanjo hiyo itaimarisha afya ya mifugo, kuongeza thamani ya mazao yake na kuifanya iwe na soko ndani na nje ya nchi. Pia itapunguza migogoro inayotokana na uhamaji holela wa wafugaji wanaotafuta malisho.

Bagamoyo. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema hatua ya Serikali kuanza kampeni ya chanjo ya mifugo inalenga kutatua changamoto sugu zinazowakabili wafugaji, ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika, migogoro na wakulima na wizi wa mifugo.

Akizungumza Julai 9, 2025 katika uzinduzi wa chanjo hiyo kwa Mkoa wa Pwani uliofanyika katika Kijiji cha Miono, Wilaya ya Bagamoyo, Dk Kijaji amesema kuwa chanjo hiyo ni mwanzo wa mageuzi katika sekta ya mifugo nchini.

“Chanjo hii itaimarisha afya ya mifugo, kuongeza thamani ya mazao yake na kuifanya iwe na soko la ndani na nje ya nchi. Pia itapunguza migogoro inayotokana na uhamaji holela wa wafugaji wanaotafuta malisho,” amesema Dk Kijaji.

Ameongeza kuwa Serikali tayari imeanza kutenga bajeti kwa ajili ya kuanzisha na kuboresha miundombinu ya huduma za mifugo, katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa shughuli hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga amesema kuwa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada za pamoja za Serikali, viongozi wa vijiji na kamati za ulinzi na usalama.

“Bagamoyo tulikuwa tunalalamikiwa sana kwa migogoro ya ardhi, lakini hali imebadilika. Chanjo hii ni nyongeza ya suluhisho kwa sababu wafugaji watapunguza kuhamahama,” amesema Ndemanga.

Amesema kuwa mkoa huo unatarajia kuchanja jumla ya ng'ombe 697,320 mbuzi 273,292 kuku 3,187,097 na Nguruwe 26,895 na shughuli hiyo itafanyika kwa siku 30.

"Mfugaji atagharamia chanjo kwa kushirikiana na  Serikali kwa upande wa ng’ombe, mbuzi na nguruwe lakini kwa upande wa chanjo ya kuku Serikali itagharimia kwa asilimia 100," amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Ngobere Mfamau amepongeza uamuzi wa Serikali kuanzisha kampeni hiyo akisema kuwa itachochea maendeleo ya sekta ya mifugo.

Farida Mnyami mkazi wa Kijiji cha Miono amesema kuwa ujio wa chanjo hiyo unaokwenda sanjali na uvalishwaji wa hereni kwa mifugo, utawaondolea changamoto ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.

"Hereni wanazovalisha ng'ombe za utambuzi kuanzia mmiliki na eneo analoishi hivyo hata mfugaji akilisha mifugo yake kwenye shamba la mkulima inakuwa rahisi kutambulika na hatua kuchukuliwa," amesema.