Odinga amtaka Rais Ruto kuacha kumchafua

Muktasari:

  • Kiongozi wa Azimio la Umoja nchini Kenya amemtaka Rais William Ruto kuacha kumchafua katika ziara zake nje ya nchi na badala kutatua matatizo ya Wakenya.

Kenya. Kiongozi wa Azimio la Umoja nchini Kenya amemtaka Rais William Ruto kuacha kumchafua katika ziara zake nje ya nchi na badala kutatua matatizo ya Wakenya.

Akiongea leo Jumatano, Raila amesema badala ya Ruto kumchafua ni vema akazingatia kutatua changamoto zinazowakumba Wakenya, alizoziacha nchini humo na kwenda nje na kusema kwamba hivyo ndivyo Wakenya wanavyotaka afanye.

"Hakuna haja ya William Ruto kwenda Ujerumani kunisema vibaya. Rudi nyumbani kutatua matatizo ya wananchi. Acha kupiga kelele nje ya nchi, njoo hapa na ufanye kile ambacho Wakenya wanataka ufanye," amesema Odinga.

Alizungumza baada ya mkutano na Jumuiya ya Wanubi na wawakilishi wa Kanisa huko Kibra, ambapo walitoa wito wa kusitishwa, kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa Jumatatu.

Matamshi hayo yanakuja baada ya Ruto aliyezungumza katika mkutano na Wakenya wanaoishi Ujerumani kusema ni lazima Wakenya wote watii sheria.

Aliongeza kuwa atahakikisha maisha, mali na biashara ya kila mtu zinalindwa.

"Hilo ndilo linalotufanya kuwa sawa. Hakuna mtu anayepaswa kukandamiza haki za wengine," alisema.

"Tumewapa polisi uhuru wa kiutendaji na kifedha kwa makusudi kufanya kazi. Ni jukumu lao kuhakikisha kila mtu anafuata utawala wa sheria."

Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano nchini humo, Eliud Owalo katika mkutano na wanahabari kwa niaba ya serikali aliushutumu muungano wa Azimio la Umoja kwa kukataa kukubali kushindwa licha ya kushindwa katika uchaguzi.

Alisema wanatumia gharama za maisha kuwa njama kufanikisha ajenda zao huku wakipuuza misingi ya katiba.