Odinga awataka wafuasi wake kususia kula mayai

Muktasari:

  • Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amewataka wafuasi wake kususia kula mayai ambayo yanazalishwa na kampuni za Kenya zinazojihusha na serikali inayoongozwa na Rais William Ruto ikiwa ni moja ya harakati zake za kupingana na serikali.

Kenya. Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ametangaza kampeni ya kuanza kususia bidhaa kutoka baadhi ya kampuni za nchini humo zinazojihusisha na serikali inayoongozwa na Rais William Ruto.

 Odinga amesema kampuni hizo zimekuwa zikishirikiana na utawala wa Kenya Kwanza kuwahujumu wafuasi wa Azimio na kuwataka wafuasi hao kususia ulaji wa mayai kama njia ya kuonyesha uasi wao dhidi ya utawala wa Rais Ruto.

Akiongea na wafuasi wake kwenye mkutano wa hadahara uliofanyika katika kaunti ya Migori Machi 10, Odinga aliweka wazi wanaanza kampeni za kukataa bidhaa moja baada ya nyingine na huduma za kampuni zinazohusishwa na serikali ya nchini humo.

"Mayai, mayai tutawaambia hii bidhaa muachane nayo hadi siku tutakayowambia muanze kula tena, hata redio tutawaambia, gazeti tutawaambia msisome hii," alisema Raila.

Aliongeza kuwa kuna orodha ya kampuni ambazo Azimio itagoma kutumia huduma na bidhaa zake kwa kuwa na ushirika na utawala wa Kenya Kwanza. "Kuna kampuni kadhaa ambazo tunajua zinatumiwa vibaya, na sasa tutawaambia hii makampuni msitumie," alisema Raila.

Hii inatokana na Rais Ruto kujihusisha na ufugaji wa kuku katika shamba lake la Sugoi ambapo amewahi kusema hufanya biashara kubwa ya kuuza mayai.

Marufuku hiyo ya kununua mayai imetolewa na Waziri Mkuu huyo mstaafu miezi michache tangu afanye maandamano ya kupinga kupaa kwa bei za bidhaa na wafuasi wake wa Azimio la Umoja.

Huku wachambuzi wa siasa za Kenya wakihusisha na agizo la Rais Ruto kuruhusu soko huru katika uwekezaji wa gesi ya kupikia na maziwa.

Aidha upande mwingine kwenye mtandao wa Twitter kauli hiyo ya Odinga imepata upinzani mkali kutoka kwa Mwanasheria wa Kenya, mchapishaji na mwandishi wa safu za magazeti, Ahmed nasir baada ya kuposti picha ikimuonyesha Odinga akila mayai, akiandika kuwa mayai yanaprotini nyingi.

Wakili huyo amemsihi Raila Odinga kutambua kuwa mayai yana protini nyingi na hayawezi kutumika kama silaha ya kulipiza kisasi kisiasa na kumtaka kiongozi huyo kutekeleza siasa safi kinyume na mtindo mbovu na ambao haujakomaa wa siasa.

“Katika siku zijazo, viongozi wa serikali lazima wafuate sera zinazonufaisha watu” amesema wakili Ahmed nasir.