Papa awaambia waumini ‘bado yupo hai’

Papa Franscis aruhusiwa kutoka hospitalini, baada ya kutoka asema "bado yuko hai" akimaanisha watu wasiwe na hofu juu ya afya yake.

Hatimaye kiongozi mkuu wa Kanisa la Katoliki duniani, Papa Francis ameruhusiwa kutoka hospitali ambapo alilazwa kwa siku tatu.

Kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa duniani baada ya kutoka hospitalini aliwaambia waandishi wa habari na waumini kwamba "bado yuko hai," akimaanisha wasiwe na hofu juu ya afya yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari ‘BBC’ walieleza kwamba Papa alilazwa katika Hospitali ya Gemelli katikati ya wiki akiwa na matatizo ya kupumua na baadaye kugundulika kuwa na ugonjwa wa mkamba.

Taarifa kutoka Vaticani ilieleza kwamba papa alikuwa akitumia dawa huku wakiamini kuwa ataruhusiwa siku ya Jumamosi, kulingana na matokeo ya vipimo.

Wanaeleza mara baada ya kutoka hospital papa alionekana akitabasamu na kupunga mkono kutoka kwenye gari, kabla ya kutoka nje kuzungumza na umati wa wa watu na kisha kuelekea Vatican.

Kulazwa kwa Papa hospitalini kulijitokeza kabla ya wiki yenye shughuli nyingi zaidi katika kalenda ya Kikristo kuadhimisha Pasaka.

Wiki Takatifu, kama inavyojulikana, inajumuisha ratiba yenye shughuli nyingi ya matukio na huduma ambazo zinaweza kuhitaji mahitaji ya kimwili.

Msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema Ijumaa kwamba Papa alitarajiwa kushiriki katika ibada ya wikiendi hii kwa Jumapili ya Mitende.

Papa huyo mwenye utaifa wa Argentina, aliadhimisha miaka 10 kama mkuu wa Kanisa Katoliki mapema mwezi huu. Kiongozi huyo wa kiroho amekabiliwa na matatizo kadhaa ya afya, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa sehemu ya pafu lake akiwa na umri wa miaka 21.

Pia ametumia kiti cha magurudumu katika miezi ya hivi karibuni kwa sababu ya matatizo yanayohusiana na goti lake.

Lakini Papa ameendelea kufanya ziara maeneo mbalimbali na hivi karibuni alitembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Pia mwezi uliopita, aliongoza mazishi ya mtangulizi wake Papa Benedict XVI.


Imeandaliwa na Emmanuel Msabaha.