Raia wa Ireland avunja rekodi akipika kwa siku nane

Dar es Salaam. Ikiwa ni miezi sita sasa tangu mpishi maarufu kutoka Nigeria, Hilda Baci kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness kwa kupika siku nne mfululizo (saa 100) hatimaye rekodi hiyo imevunjwa na Alan Fisher baada ya kupika kwa siku nane sawa na saa 199.

Baci alitangazwa rasmi kuvunja ‘rekodi’ na Guiness World Records mwezi Mei mwaka huu baada ya kupika vyakula tofauti tofauti kwa saa 100 bila ya kupumzika.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa katika akaunti ya mtandao wa X ya Guiness World Records leo Jumanne Novemba 7,2023 inaeleza kuwa  Fisher ambaye ni raia wa Ireland, mpishi na mmiliki wa mgahawa mmoja nchini Japan amefanikiwa kupika kwa saa 199 na dakika 57.

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa pamoja na kumpiku Bacci, Fisher anashikilia rekodi ya kuoka mkate kwa muda mrefu kwa kutumia takribani saa 47 na dakika 21.

Rekodi hiyo awali ilikuwa ikishikiliwa na Wendy Sandner kutoka Marekani baada ya kuoka mkate kwa muda wa saa 31 dakika 16.

Baada ya kutangazwa rasmi kwa Fisher kuvunja rekodi hiyo, Bacci ambaye alikuwa akishikilia rekodi hiyo awali kupitia mtandao wa X amempongeza Fisher na kumtakia kila la heri.

"Hongera sana Alan Fisher ni mafanikio makubwa, na ninamtakia kila la heri kama mmiliki mpya wa rekodi hiyo ya dunia," amesema.