Ruto na Odinga walegeza misimamo

Rais wa Kenya, William Ruto akiwa na hasimu wake, Raila Odinga katika moja ya hafla siku za nyuma. Wanasiasa hao wameamua kulegeza misimamo yao na sasa wanaweza kukaa meza moja kwa mazungumzo.

“Je, meza imepinduliwa.” Hivyo ndivyo unaweza kujiuliza baada ya Rais, William Ruto kusema yuko tayari kushirikisha pande mbili bungeni kwa ajili ya kuundwa upya kwa Tume huru ya Uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC).

Mbali na Ruto kulegeza msimamo, pia, kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga naye amekubali kulegeza msimamo wake kwa kukubali kusimamisha maandamano na kuzungumza na Serikali.

Miongoni mwa malalamiko ya Azimio la Umoja-One Kenya, wanataka mabadiliko IEBC hasa namna ya uteuzi wa makamishna wake.

Ruto ambaye anasisitiza uhusiano wake na Wakenya wa kawaida kwa kujiita “hustler”, (mpiga mbizi) alishinda kwa kupata kura 7,176,141 (asilimia 50.49) dhidi ya kura 6,942930 (asilimia 48.85) alizopata mpizani wake Odinga ambaye wafuasi wake wanamuita “Baba”.

Kilichosababisha ‘the handshake’ ya Kenyatta na Odinga pamoja na maandamano, pia Odinga alijiapisha kuwa ‘rais wa wananchi wa Kenya.’


Alichosema Ruto

Akihutubia Taifa juzi, Rais Ruto, ambaye siku zote tangu kuapishwa kwake Septemba 13, 2022 amekuwa akihubiri kukataa maridhiano ya kushikana mkono, maarufu ‘the handshake’ na Odinga, lakini hotuba yake ya juzi ni kama amepindua meza na kukubali mkono wa maridhiano ‘hand reconciliation’.

IEBC ni moja ya hoja za Azimio la Umoja kufanya maandamano ya takriban wiki mbili na kusababisha vifo, majeruhi, kuzuia shughuli mbalimbali za kibiashara, elimu na upotevu wa mali.

Ruto hakutaka kurejea maridhiano ya kisiasa na upinzani kama yaliyowahi kufanywa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ya kushikana mkono na Raila Odinga, maarufu ‘the handshake’ uliofanyika Machi 9, 2018, kwenye ukumbi wa Harambee House.

‘The handshake’ ilimfanya Odinga kuwa karibu na Serikali ya Rais Kenyatta huku Ruto akiamua kujiweka pembeni na Serikali na kuna wakati alibadilishiwa walinzi na bajeti ya ofisi yake iliondolewa.

Pia, Ruto hakutaka maridhinao kama yaliyofanyika mwaka 2008 yaliyomuingiza Odinga kwenye nafasi ya Waziri Mkuu chini ya Rais Mwai Kibaki.

Hata hivyo, juzi akihutubia Taifa kutoka Ikulu ya Nairobi, alitoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa pande mbili bungeni kuhusu kuundwa upya kwa IEBC, mojawapo ya masuala muhimu yaliyochangia wito wa maandamano ya Azimio la Umoja nchini kote kupinga Serikali.

“Ninapendekeza ushirikiano wa pande mbili bungeni kuhusu uundaji upya wa jopo la IEBC ndani ya vigezo vya sheria na katiba,” alisema Ruto.

Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na upande wa Azimio la Umoja wakisema hiyo ni hatua nzuri kwao na kutaka wajumbe watakaunda ushirikiano huo bungeni wateuliwe haraka.

“Tuko tayari kushiriki na tutajihusisha bila aina yoyote ya rushwa na mchakato huu unapaswa kuanza mapema kesho (jana),” ilikuwa ni kauli ya Odinga aliyekuwa amekuwa ameongozana na viongozi wenzake wa Azimio la Umoja.

Maandamano ya Azimio la Umoja kwa takriban wiki mbili yalikuwa na hoja ya gharama ya maisha, uteuzi wa makamishana wa IEBC , ukosefu wa uwazi katika mfumo wa uchaguzi na idara ya usalama kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabili wanadamanji.


Sifa mbaya

Ruto akihutubia Taifa alisema maandamano hayo yanaichafua nchi ya Kenya huku wahuni wakiyatumia kuharibu na kuiba mali za watu.

“Katika wiki mbili zilizopita, watu wamekufa, kujeruhiwa, mali kuibwa au kuharibiwa, uchumi umeathiriwa vibaya na heshima yetu kama nchi imetiwa doa,” alisema.

Ruto alisema ingawa polisi wamefanya kila wawezalo kulinda maisha na mali ya raia, ghasia zimeendelea kuvuruga mageuzi ya uchumi ya Serikali yake.

“Nimesikiliza masuala anayozua rafiki yangu, mheshimiwa Raila Odinga. Katika hali kama ilivyo, sio kuhusu aliye sahihi na asiye sahihi,” alisema Rais Ruto.

Akaongeza: “ Nimekuwa tayari kujadiliana na Wakenya wa matabaka yote, wakiwemo viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa kutoka mirengo yote ya kisiasa na viongozi wa kidini kuhusu jinsi ya kufanya nchi yetu kuwa bora na yenye ustawi.

“Milango yangu ingali wazi kwa mazungumzo ya wazi, nia njema kwa misingi ya sheria na katiba,” alisema.

Pia, Ruto alikubaliana na hoja ya Odinga ya mchakato wa kupata makamishna wa IEBC upitie bungeni kwa njia isiyoegemea upande wowote.

“Kwa kuzingatia masuala ambayo yamezuliwa kuhusu hili, ninapendekeza mazungumzo ya pande zote katika Bunge kuhusu kuundwa upya kwa jopo la kuajiri makamishna wa IEBC ndani ya misingi ya kisheria na katiba,” alisema Ruto.

Odinga amekuwa akitoa madai kuwa uteuzi wa makamishna wa IEBC unaofanywa na Rais Ruto umelenga kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.


Muundo wa kamati

Pia, Odinga anataka kamati ya Bunge ya kujadili mageuzi ndani ya IEBC, iwe na wenyeviti wawili kutoka upande wa Azimio na Kenya Kwanza.

Odinga pia kwenye hotuba yake anataka wataalamu wa kimataifa wajumuishwe katika kamati hiyo.

“Kamati hiyo ya Bunge iundwe mara moja na kuanza mazungumzo,” alisema Odinga.

Pia, Odinga katika masharti yake ametaka makamishna wanne wa IEBC waliojiuzulu kutokana na shinikizo la Serikali warejeshwe kazini.


Siasa za Kenya

Siasa za Kenya kwa miaka mingi kila unapomalizika uchaguzi mkuu wa rais kumekuwa na machafuko yanayoilazimu nchi hiyo kwenda kwenye maridhiano.

Hata hivyo, kabla ya ‘the handshake’ ya mwaka 2018 kati ya Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, matokeo ya Rais ya mwaka 2007, yalisababisha mzozo wa kisiasa baada ya ushindi wa Mwai Kibaki kugomewa na mpinzani wake Raila Odinga na kuzusha vurugu zilizosababisha watu 1,500 kupoteza maisha wengine zaidi ya 600,000 kupoteza makazi yao.

Vurugu hizo zilisababisha watuhumiwa sita waliodaiwa kufadhili machafuko hayo kushtakiwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na mwendesha mashtaka mkuu, Luis Moreno-Ocampo.

Washtakiwa walikuwa sita na kuifanya kesi hiyo kuwa maarufu kwa kuitwa ‘Ocampo Six’, miongoni mwa washitakiwa hao ni aliyekuwa Waziri wa Elimu, William Ruto, mtangazaji wa redio host Joshua Sang, Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura.


Juhudu za upatanashi

Juhudi za kwanza za upatanishi zilifanywa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa Ghana John Kufuor kwa kuwakutanisha Kibaki na Odinga, huku sharti likiwa kumtaka Odinga asitishe maandamano na hilo lilifanyika.

Hata hivyo, Odinga alikataa kufanya mazungumzo ya amani na Kibaki pekee yao, akitaka yawe ni sehemu ya maridhiano ya kimataifa kwa ushiriki Rais Kufuor.

Hata hivyo, upatanishi uliendelea chini ya alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na aliyekuwa Rais wa Tanzania kwa wakati huo Jakaya Kikwete.

Mazungumzo hayo yaliweza kuzaa makubaliano ya kuunda Serikali ya pamoja na Odinga akawa Waziri Mkuu huku Kibaki akiendelea kushika kiti cha urais.