Saa 24 zilivyomtikisa Vladimir Putin, Ulaya

Baadhi ya askari wa kundi la mamluki la Wagner wamekaa juu ya kifaru baada ya kuvuka mpaka wa Ukraine wakielekea Russia kwa kile wanachodai kwenda kutekeleza maandamano ya kupigania haki. Picha na mtandao

Juni 24 mwaka huu, Rais Vladimir Putin wa Russia aliingia katika kile kilichoonekana kuwa ni mzozo kati ya Serikali yake na jeshi binafsi la Wagner, akilituhumu kwa usaliti na uhaini.

Siku hiyo ilionekana kuwa ndefu kwa Putin baada ya kiongozi wa mamluki wa Russia, Yevgeny Prigozhin kuanzisha kile kilichoonekana kama uasi na kutuma wapiganaji wake kuelekea Moscow na kuibua maswali juu ya mamlaka na nguvu za Vladimir Putin madarakani.

Lakini kabla siku hiyo haijamalizika, wakiwa umbali mfupi kufika Moscow, Prigozhin alibadilisha mwelekeo na kuwaamuru wapiganaji wake kurejea kambini.
Kitendo cha kubadilisha mwelekeo kiliwafanya wengi wajiulize maswali kuhusu hatua hiyo.

Wengine walisema ule haukuwa uasi bali ni mchezo wa Putin na Prigozhin wa kuwachanganya watu wa nchi za Magharibi na Ukraine, na kwamba kitendo cha kuivamia Rostov kilikuwa kama igizo tu, kwa sababu wanajeshi wa Russia hawakuonyesha upinzani wowote na hivyo hakukuwa na mapigano yoyote yaliyoripotiwa.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Prigozhin kuudanganya ulimwengu.
Ni kama vile alivyowahi kusema kuwa anawaondoa wapiganaji wake huko Bakhmut, lakini siku 10 baadaye akaiteka.

Vita vya Bakhmut vimeonyesha kwamba Prigozhin anaweza kusema jambo A lakini akatenda C.

Kwa miezi kadhaa, amekuwa akitekeleza jukumu muhimu katika kampeni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine, akiandikisha maelfu ya watu kwa kundi lake la mamluki la Wagner, hususani kutoka jela za Russia.

Muda mrefu sasa amekuwa katika mzozo wa wazi na wakuu wa kijeshi wa Russia wanaoendesha vita, lakini hilo liligeuka kuwa uasi wa wazi walipoanza kuandaa mpango wa kuwadhibiti wapiganaji wake ifikapo Julai mosi mwaka huu.

Baadaye siku hiyo Prigozhin alisisitiza kuwa hayo yalikuwa ‘maandamano ya haki’ na si mapinduzi. Lakini vyovyote ilivyokuwa, yaliisha haraka sana kama yalivyoanza.
Zilikuwa ni saa 24 za taharuki kwa Serikali ya Russia. Ndani ya muda wa siku moja tu, matukio yaliongezeka na kisha yakapungua haraka.

Ndani ya siku hiyohiyo moja Wagner walikomesha uasi waliouanzisha wao wenyewe.
Siku moja kabla, Ijumaa ya Juni 23, Prigozhin alitema cheche akimlaumu Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu, kutokana na vita vya Ukraine, akidai alifanya hivyo ili kupata heshima ya kijeshi.

Prigozhin baadaye aliapa ‘kuandamana kwa ajili ya haki’ na kumshutumu Putin kwa kuwashambulia wanajeshi wake kwa shambulio la kombora.
Ijumaa hiyohiyo usalama uliimarishwa mjini Moscow, baada ya Prigozhin kutoa wito wa uasi wa kutumia silaha.

Mapema asubuhi ya Jumamosi, Prigozhin alitangaza kuwa wanajeshi wake 25,000 wamevuka mpaka kutoka Ukraine kuingia Russia.

Meya wa Moscow alitangaza kuwa hatua za kupambana na ugaidi zinachukuliwa ili kuimarisha usalama huko Rostov-on-Don, karibu na mpaka wa Ukraine, na wakazi wa eneo hilo waliamriwa kukaa ndani.

Muda mfupi kabla ya saa 12 asubuhi kwa saa za Russia, video ilionekana mtandaoni ikimwonyesha Prigozhin akiwa ndani ya makao makuu ya kijeshi ya kusini mwa Russia.
Saa 2:00 asubuhi kwa saa za Russia, Rais Putin alionekana akilihutubia taifa lake kwa njia ya televisheni akishutumu ‘matukio ya uhalifu’, na kuonya kuwa adhabu kali itatolewa kwa wahusika na kuapa kuwalinda wananchi wake dhidi ya uvamizi.

Wakati Rais Putin akilihutubia taifa lake, vikosi vya Wagner vilikuwa vinasonga mbele kwenye Barabara ya M4 kuelekea Moscow, pamoja na kukamata vifaa vya kijeshi huko Voronezh.

Lakini kabla ya saa 12:30 jioni (saa za Russia), Prigozhin alitangaza kwamba amekubali ‘kusimamisha’ harakati za wanajeshi wake.

Kituo cha televisheni cha Belarus kilionyesha kiongozi wake, Alexander Lukashenko akifanya mazungumzo na Prigozhin na Putin alikubali mazungumzo hayo.
Karibu saa 3:00 usiku vyombo vya habari vya Serikali ya Russia viliripoti kwamba Prigozhin ataondoka kwenda Belarusi, na mashtaka ya uhalifu dhidi yake na askari wake yatafutwa.

Je, yalikuwa mapinduzi? Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, Prigozhin anasema kuwa madai yote ya mapinduzi ya kijeshi ni ‘upuuzi’.

Lakini kile kilichoanza kama mzozo juu ya jeshi la Russia kushindwa kuwapa mamluki wake vifaa vya kutosha vya kijeshi, kiligeuka na kuwa uhasama wa moja kwa moja kati ya watu wawili wanaosimamia vita vya Ukraine ambao ni Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu na Mkuu wa vikosi vya jeshi, Valery Gerasimov.

Haya hayakuwa mapinduzi kwa sababu hakukuwa na jaribio lolote la kutwaa madaraka kwa kuipindua Serikali.

Lakini ni jaribio la kuwang'oa madarakani wakuu wa jeshi la Russia na hivyo kuleta changamoto kubwa kwa mamlaka ya rais.

Jiji zima la Moscow liliwekwa katika hali ya tahadhari ilipoanzishwa ‘operesheni ya kukabiliana na ugaidi’ na matukio makubwa yalishuhudiwa kufuatia hatua hiyo.
"Kuna 25,000 kati yetu," alidai Prigozhin. "Yeyote anayetaka anaweza kujiunga nasi".
Wito huo haukutosha kumtisha rais lakini ni changamoto kwa uongozi wa kijeshi.

Kwa muda mrefu, Prigozhin amekuwa mshirika wa karibu sana wa Rais Putin na amestawi sana chini ya utawala wake, kwanza akiwa mfanyabiashara tajiri na baadaye kama mkuu wa kundi la mamluki.

Wapiganaji wa Wagner wamekufa kwa wingi katika mapambano makali ya kuiteka Bakhmut mashariki mwa Ukraine, ambayo yalidumu kwa miezi kadhaa na hayakufanikiwa kikamilifu.

Prigozhin anawalaumu wakuu wa kijeshi kutokana na uhaba wa makombora, akiweka mitandaoni video zinazofichua kasoro za jeshi la Russia nchini Ukraine.
Hakuelekeza moja kwa moja hasira yake kwa rais, lakini kauli zake zinaonekana kumkosoa Rais Putin kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Juni 23, ikiwa ni siku moja kabla ya wapiganaji wake kuingia Russia, aliwaambia raia wa nchi hiyo kuwa vita vyao dhidi ya Ukraine havina msingi wowote na kwamba limeanzishwa ‘kundi dogo la wahuni’.

Tangu wakati huo hali imeendelea kubadili kwa haraka sana.
Prigozhin alilishutumu jeshi la Russia kwa kuwashambulia watu wake huko Ukraine, lakini jeshi lilikanusha na hajatoa ushahidi wowote kama anavyofanya mara kwa mara.
Ndipo siku hiyohiyo, Ijumaa ya Juni 23, akatangaza hatua yake ya ‘kupigania haki’.
Akavuka mpaka wa Ukraine na kuingia Russia akiwa na wapiganaji wake 25,000.

Jenerali Sergei Surovikin, naibu kamanda wa vikosi vya Ukraine, alimwomba arudi nyuma na kutii mamlaka ya Rais Putin.

Lakini kufikia asubuhi wapiganaji wa Prigozhin walikuwa wamefika Rostov na kutangaza: "Tuko ndani ya makao makuu ya kijeshi".

Hakutishia tu kuweka kambi huko Rostov, bali kuelekea Moscow ikiwa matakwa yake ya kijeshi hayatatekelezwa.
Ingawa ni mapema sana kusema mzozo huu utaisha lini na utaishia wapi, swali muhimu ni je, huyu Prigozhin ni nani?

Yeye ni nani katika kundi la Wagner? Na kundi la mamluki la Wagner lilianzishwa lini na nani, na kwa nini limekuwa tishio sana, hususani kwa Russia yenyewe?
Kundi la Wagner lina ofisi katika nchi 20 za Afrika, miongoni mwa hizo ni Eswatini, Lesotho na Botswana na lina wapiganaji katika nchi kadhaa duniani.


Linapata wapi nguvu hizo?
Kuyajua haya na mengine mengi, tukutane kesho kwa simulizi zaidi kuhusu Kundi la Wagner.