Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu EU kupinga mkakati wa Marekani kuidhoofisha ICC

Muktasari:

  • Marekani imeingia katika mvutano na Jumuiya ya Ulaya (EU) baada ya kuanzisha kampeni ya kuidhoofisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ikidai inaleta tishio kwa mamlaka yake. Hatua hiyo imekosolewa na EU, ambayo imeitaja ICC kuwa muhimu katika kulinda uwajibikaji dhidi ya uhalifu dhidi ya binadamu duniani.

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU) umepinga mpango wa Serikali ya Marekani wa kuchukua hatua dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (International Criminal Court - ICC), ukisema mahakama hiyo haiwakilishi tishio kwa mamlaka ya nchi, bali ni chombo muhimu cha kuhakikisha watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa wanawajibishwa.

Mvutano huo umeibuka baada ya Serikali ya Marekani kutangaza kampeni ya kuishinikiza na kuidhoofisha ICC, mahakama yenye makao yake The Hague, Uholanzi, ikidai kuwa taasisi hiyo inaingilia mfumo wake wa kisheria na kisiasa. Hatua hiyo imeibua mjadala kuhusu mpaka kati ya mamlaka ya nchi na wajibu wa kimataifa wa kulinda haki.

Katika kukabiliana na hatua hiyo, Msemaji wa Umoja wa Ulaya, Anouar El Anouni, amesema EU itaendelea kuunga mkono ICC na kupinga vitisho vinavyolenga mahakama hiyo, viongozi wake au watu wanaoshirikiana nayo.

"EU inasimama imara katika kuunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Mashambulizi au vitisho dhidi ya mahakama, viongozi waliochaguliwa, wafanyakazi wake au wale wanaoshirikiana nayo havikubaliki," amesema El Anouni katika tamko la jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa EU, moja ya sababu kuu za kupinga hatua za Marekani ni kwamba ICC hailengi kuvunja mamlaka ya nchi kama ambavyo Washington inadai, bali inalenga kuwawajibisha watu binafsi wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa unaohusu jumuiya ya kimataifa.

"ICC hailengi mataifa huru wala haitoi tishio kwa mamlaka zao. Badala yake, inatumia mamlaka yake dhidi ya watu wanaohusika na uhalifu mkubwa unaohusu jamii ya kimataifa," amesema El Anouni.


Kwa nini Marekani inaipinga ICC?

Serikali ya Marekani imeibua kampeni yake hiyo ikiikosoa Mahakama ya ICC kuwa inatishia mamlaka ya nchi huru na kwamba inaweza kutumika kuwafikisha mahakamani viongozi wake au maafisa wa serikali kwa maamuzi yanayofanywa katika kutekeleza majukumu yao.

Katika mpango huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema mahakama hiyo inatishia mfumo wa kisiasa na kisheria wa Marekani.

"Mahakama hii inatishia kila sehemu ya mfumo wetu wa kisiasa na kisheria," amesema Rubio.

Katika maelezo yake, licha ya Marekani kutokuwa mwanachama wa mahakama hiyo, Rubio alieleza hofu kwamba viongozi wa Marekani, maafisa wa ulinzi wa mipaka na watendaji wengine wanaweza kufikishwa mbele ya majaji wa kimataifa katika mahakama hiyo.

Katika mkakati wa kufanikisha lengo hilo, Marekani ilisema itachukua hatua mbalimbali dhidi ya ICC, ikiwemo kuishinikiza baadhi ya nchi kujiondoa katika mahakama hiyo na kuongeza uangalizi kwa nchi zitakazokataa kufanya hivyo huku zikitumia msaada wa Marekani.


Sababu EU kuilinda ICC

EU inaona hatua hizo zinaweza kudhoofisha mfumo wa kimataifa wa uwajibikaji uliowekwa ili kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na uhalifu wa uchokozi.

Kwa mtazamo wa Umoja huo, ICC ni chombo cha mwisho pale ambapo mifumo ya ndani ya nchi imeshindwa au haitaki kuwachunguza na kuwawajibisha wahusika wa uhalifu mkubwa.

Katika mtazamo huo huo wa EU, naye Kenneth Roth, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Human Rights Watch, alisema madai ya Marekani yanapotosha nafasi ya ICC.

"ICC haidai kuwa na mamlaka juu ya vitendo vinavyofanyika ndani ya Marekani. Rubio anafunika juhudi za kutafuta kutokuwajibika kwa uhalifu wa kivita wa Marekani kwa jina la mamlaka ya kitaifa," alisema Roth.


ICC ilianzishwa kwa lengo gani?

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilianzishwa mwaka 2002 baada ya kuanza kutumika kwa Mkataba wa Roma wa mwaka 1998. Makao makuu ya ICC yako The Hague, Uholanzi, na kazi yake kubwa ni kuchunguza na kushtaki watu wanaodaiwa kuhusika na uhalifu mkubwa zaidi duniani.

Mahakama hiyo hushughulikia makosa manne makubwa; mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na uhalifu wa uchokozi, ambapo shughuli zake si kuendesha kesi dhidi ya serikali, bali dhidi ya watu binafsi wanaotakiwa kuwajibika kwa vitendo hivyo.

Tangu kuanzishwa kwake, ICC imeendesha kesi kadhaa kubwa duniani, zikiwemo kesi dhidi ya viongozi wa Kenya kufuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007/2008, ambapo baadhi ya mashtaka dhidi ya viongozi, akiwemo William Ruto na Uhuru Kenyatta, yalisitishwa baadaye kutokana na changamoto za ushahidi.

Mahakama hiyo pia iliwahi kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mwaka 2023 kutokana na tuhuma zinazohusiana na uhamishaji haramu wa watoto kutoka Ukraine wakati wa vita vya Urusi na Ukraine.