Spika wa Bunge Marekani aondolewa madarakani

Spika wa Bunge la Marekani aliyeondolowa madarakani, Kevin McCarthy. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Bunge la Marekani limeshuhudia historia ya mara ya kwanza kumuondoa spika madarakani kwa kupiga kura za kutokuwa na imani naye jana usiku Jumanne Oktoba 3, 2023.
Marekani. Bunge la Marekani limeshuhudia historia ya mara ya kwanza kumuondoa spika madarakani kwa kupiga kura za kutokuwa na imani naye jana usiku Jumanne Oktoba 3, 2023.
Vuguvugu la kumtimua spika wa bunge hilo, Kevin McCarthy lilishinikizwa na wabunge wa chama cha Democratic ambao kwa idadi ni wachache lakini walifanikiwa kuwashawishi na baadhi ya wabunge wa chama cha Republican kupiga kura ya kumkataa spika huyo.
Kura 216 dhidi ya 210 zilifanikiwa kumng’oa McCarthy madarakani huku wabunge wa chama chake cha Republican wanane wakiongeza idadi ya kura za kumuondoa.
Hata hivyo baada ya mchakato huo McCarthy amewaambia wanahabari kwamba hatagombea tena uspika.
"Nilipigania kile ninachoamini," McCarthy amesema. "Naamini naweza kuendelea kupigana, lakini labda kwa namna tofauti."
Vuguvugu la kumuondoa spika huyo liliongozwa na Mbunge Matt Gaetz wa chama cha Republican mwenye siasa za mrengo wa kulia kutoka Florida na mpinzani wa McCarthy.
Reuters imeripoti kuwa wadau wa demokrasia wanasema McCarthy alipoteza uaminifu wake baada ya kuvunja makubaliano kuhusu matumizi ya Serikali.
Hata hivyo, mbunge aliyeongoza harakati za kumtoa spika, Gaetz amekanusha kuwa amefanya hivyo kwasababau hampendi McCarthy.
"Huu sio ukosoaji wa mtu binafsi - ni ukosoaji wa kazi. Kazi haijafanywa," amesema.