Spika wa Bunge Somalia ajiuzulu

Muktasari:

  • “Tulikuwa ndani ya jengo la bunge asubuhi hii tukiwa tayari kwa ajili ya kupigia kura hoja ya kutokuwa na imani na spika. Mara akaingia naibu spika na akatusomea barua ya kujiuzulu kwa spika,” mbunge Dahir Amin Jesow ameliambia shirika la Reuters.

Spika wa Bunge la Somalia Mohamed Sheikh Osman Jawari amejiuzulu muda mfupi kabla ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, amesema mbunge mmoja na hivyo kuhitimisha mvutano wa kisiasa wa wiki kadhaa.
“Tulikuwa ndani ya jengo la Bunge asubuhi hii tukiwa tayari kwa ajili ya kupigia kura hoja ya kutokuwa na imani na spika. Mara akaingia naibu spika na akatusomea barua ya kujiuzulu kwa spika,” mbunge Dahir Amin Jesow ameliambia Shirika la Reuters.
Punde mwenyekiti wa kamati ya masuala ya Katiba, Abdirahman Hosh Jibril akatuma ujumbe kwa twitter.
“Tulishangilia sana na kung’atuka kwake kumekubaliwa kwa mujibu wa katiba. Huu ndiyo mwisho wa mgogoro wa kisiasa.”
Awali Jawari aligoma kuitikia wito wa kumtaka ang’atuke akisema, “Mimi sifanyi kazi kwa ajili yao, siwezi kujiuzulu.”
Mgogoro huo, ambao ulichochewa na shutuma za matumizi mabaya ya mamlaka na kuzuia mageuzi ya kikatiba dhidi ya Jawari, uligonganisha mhimili wa serikali na bunge kwa wiki kadhaa.
Jawari ameshikilia nafasi hiyo tangu Agosti 2012 na alivutana na wabunge wengine juu ya suala la hoja ya kumshtaki aliyekuwa rais wa wakati huo Hassan Sheikh Mohamud mwaka 2015.
Somalia imekuwa haifuati sheria tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya dikteta Mohammed Siad Barre kuondolewa madarakani na wababe wa vita.