Tisa wauawa shambulio Mogadishu
Wakaazi wakiwa wamekusanyika nje ya Mkahawa wa Pearl Beach kufuatia shambulio la wanamgambo wa Al Shabaab kwenye ufukwe wa Liido huko Mogadishu, Somalia Juni 10, 2023
Muktasari:
- Watu tisa wameuawa katika shambulio lililodaiwa na wanamgambo wa Kiislamu wa al Shabaab katika mgahawa wa soko katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu jana Ijumaa usiku, polisi wamesema.
Mogadishu. Watu tisa wameuawa katika shambulio lililodaiwa na wanamgambo wa Kiislamu wa al Shabaab katika mgahawa wa soko katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu jana Ijumaa usiku, polisi wamesema.
Waliouawa katika mgahawa maarufu wa Pearl walikuwa raia sita na askari watatu, polisi wamesema katika taarifa. Abdikadir Abdirahman, Mkurugenzi wa huduma ya gari la wagonjwa la Aamin, amesema walibeba watu 20 waliojeruhiwa kutoka eneo la tukio.
Vikosi vya usalama viliokoa raia 84 huku hatima ya washambuliaji ikiwa haijulikani, taarifa ya polisi imesema.
Shirika la Habari la Taifa la Somalia lilisema kwenye Twitter kwamba vikosi vya usalama vimefanikiwa kuwaondoa wanamgambo wa al Shabaab waliohusika na shambulio la kigaidi kwenye Mgahawa huo huko Lido Beach, Mogadishu.
Siku ya Jumamosi, uchafu kutoka kwenye mgahawa huo ulitapakaa kwenye barabara iliyojaa damu na vioo vya dirisha vilivyokuwa vimevunjika kutokana na shambulio hilo.
Hussein Mohamed, mhudumu katika mgahawa mwingine ulio karibu, alisema alisikia mlipuko uliofuatiwa na milio ya risasi wakati shambulio hilo lilipoanza.
"Eneo lote limezingirwa na vikosi vya usalama," amesema.
Al-Shabaab yenye mafungamano na Al Qaeda imekiri kwamba ndiyo iliyohusika na shambulio hilo.
Mwezi Novemba, kundi hilo linalodhibiti maeneo mengi ya nchi, lilishambulia hoteli nyingine mjini Mogadishu, na kuwaua watu tisa.
Al Shabaab walidhibiti eneo kubwa la Somalia kabla ya kurudishwa nyuma katika mashambulizi ya serikali tangu mwaka jana. Hata hivyo, wanamgambo hao bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya shabaha za serikali, kibiashara na kijeshi.
Mwishoni mwa mwezi Mei, wapiganaji wake walishambulia kambi ya walinda amani wa Uganda kilomita 130 (maili 80) kusini magharibi mwa Mogadishu, na kuua wanajeshi 54.