Trump azindua mpango wa amani

Muktasari:

Mpango huo unahusu mataifa ya Mashariki ya kati.

Washington, Marekani. Hatimaye Rais wa Marekani, Donald Trmp ametangaza mpango wake wa amani ya Mashariki ya kati.

Mpango huo uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu utahusisha nchi za Isreal na Palestina.

Uzinduzi huo ulifaywa jana Jumanne Januari 28 mbele ya Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kiongozi wa upinzani Benny Gantz.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameutaja mpango huo kuwa ni makubaliano ya karne.

Alisema siku hiyo ni ya kihistoria sawa na ile ya Mei 14, 1948 ambako Rais wa zamani wa Marekani, Harry Truman alikuwa kiongozi wa kwanza wa kimataifa kulitambua taifa la Israel.

Kwa upande wake Rais Trump alisema ulikuwa ni mpango mgumu zaidi kuwahi kufikiwa.

Hata hivyo, Rais Trump alisema kwa pamoja wanaweza kuanza upya katika eneo la Mashariki ya kati na kuzishukuru Serikali za Oman, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa msaada walioutoa ili kufanikisha mchakato huo.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa mpango huo ni suluhisho la kweli la mataifa mawili kwa kuwa Jerusalem itasalia mji mkuu ambao hautagawanywa. Hata hivyo alisema mji mkuu wa taifa la Palestina katika siku za usoni utapaswa kuundwa na sehemu za Mashariki ya Jerusalem kupitia makubaliano ya mipaka yaliyofanana na maelezo ya maafisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani.

Alisema mpango huo pia unatoa muda wa miaka isiyozidi minne kwa Israel kusitisha ujenzi wa makazi ingawa utaruhusu taifa hilo kuendeleza udhibiti wa walowezi ambao tayari wamejenga.

Hata hivyo, mpango huo ambao umecheleweshwa kwa miaka miwili umepingwa na Wapalestina.

Maafisa wa Palestina wanadai kwamba Trump anaipendelea zaidi Isreal na kuiimarisha serikali hiyo ya Netanyahu.

 

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas kupitia taarifa yake alisema  anaikaribisha hatua hiyo na kuahidi kuifuatilia kwa karibu.

Hata hivyo Masaas alisema suluhu ya mataifa mawili na inayokubalika na pande zote ndio inatakayoleta amani ya kudumu kati ya Israel na Palestina.

Wakati mpango huo ukizinduliwa maelfu ya Wapalestina wameandamana kwenye mitaa ya Gaza na kuchoma moto picha za Trump na Netanyahu.

Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh ambaye ni mpinzani wa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas alimtaka kiongozi huyo kuahidi kuwaunga mkono kuukataa mpango huo.

Rais Abbas alishiriki mazungumzo ya awali na Israel chini ya usimamizi wa Marekani lakini baadaye alijitenga na mpango huo akidai kuwa ni njama na hautapita.