Ugomvi wa wazazi, waua mtoto wa mwezi mmoja

Muktasari:

  • Inaelezwa wazazi hao waliamka asubuhi wakiwa na ugomvi, wakati wanapigana walimuangukia mtoto wao wa umri wa mwezi mmoja na hatimaye kichanga hicho kufariki papo hapo.

Zambia. Taarifa za kusikitisha kutoka nchini Zambia zilianza kuenea wiki iliyopita baada ya mtoto wa mwezi mmoja na wiki tatu kufariki dunia baada ya wazazi wake kumwangukia wakiwa wanapigana.

Tovuti ya Diamond Tv ya nchini humo imesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Reuben Wilaya ya Shiwangandu Mkoa wa Muchinga, ambapo wazazi wa kichanga hicho waliamka asubuhi majira ya saa moja, wakiwa wanapigana ndipo walipomuangukia mtoto wao aliyekuwa amelala kitandani.

Inaelezwa muda mfupi baada ya kugundua mtoto wao amefariki waliamua kumjulisha jirani yao ambaye aliripoti kisa hicho kwa jeshi la polisi.

Baada ya kubaini uzito wa jambo hilo, wapenzi hao waliamua kukimbia nyumba na hadi sasa hawajulikani walipo.

Wazazi hao waliotambulika kwa jina la Shadrick Chanda mwenye umri wa miaka 50 na mkewe, Rebecca Mbikiloni mwenye umri wa miaka 45 kwa sasa wanasakwa na jeshi la polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Muchinga, Kaunda Mubanga amethibitisha kuwatafuta wapenzi hao.

Mwili wa mtoto huyo yapo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya Chinsali ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.