Uhusiano wa Wagner na Serikali ya Russia

Rais Vladimir Putin akimsikiliza kiongozi wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin kwenye moja ya viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali vinavyomilikiwa na kiongozi huyo mjini St. Petersburg

Tunaendelea na simulizi ya kundi la Wagner, ambalo hivi karibuni lilimnyima usingizi Rais wa Russia, Vladmir Putin. Katika toleo lililopita tuliona mwanzo wa kundi la Wagner nchini Russia. Lakini je, nini uhusiano wa kundi hilo na Serikali ya nchi hiyo? Wanachama na wapiganaji wa kundi hilo wanapatikana vipi na namna gani wanajiendesha katika shghuli zake za kila siku? Je, mzozo wa Wagner na Rais Putin una uhalisia na kama ndio unaashiria nini kwa utawala wa kiongozi huyo, ambaye kwa sasa hana mahusiano mazuri na mataifa mengi ya Ulaya? Endelea...


Juni 27, mwaka huu, zikiwa ni siku tatu tu baada ya kundi la Wagner linaloongozwa na Yevgeny Prigozhin kudaiwa kujaribu kufanya uasi, Rais Vladmir Putin alikiri kuwa lilikuwa likifadhiliwa na serikali yake.

Aliyasema hayo alipokuwa akitangaza kuanza kwa uchunguzi kuhusu matumizi ya kundi hilo. Alithibitisha kuwa Serikali yake ililifadhili kikamilifu kutoka kwenye bajeti ya ulinzi na bajeti ya Serikali.

Kuanzia Mei 2022 hadi Mei 2023 pekee Serikali ya Russia ililipa kundi hilo RUB bilioni 86.262 (takriban Sh2.3 trilioni)

Siku za nyuma mara kwa mara Putin alikanusha kuwapo uhusiano wowote kati ya Serikali yake na Wagner na kusisitiza kuwa hiyo ni kampuni ya kijeshi ya binafsi.

Kabla ya hapo, wachambuzi wengi wa siasa za kimataifa wa Russia na nchi za Magharibi waliamini kwamba kundi hilo halipo kama kampuni binafsi ya kijeshi, bali ni tawi lililojificha la mkuu Wizara ya Ulinzi ya Russia na lilikuwa likiripoti kwa Serikali ya Russia.

Kundi hilo linashirikiana maeneo kadhaa ya kijeshi na jeshi la Russia, linasafirishwa na ndege za kijeshi na hutumia huduma za afya za jeshi la nchi hiyo.

Imeripotiwa mara kadhaa na vyombo mbalimbali vya habari duniani kuwa Serikali ya Russia inaunga mkono kundi hilo, na hata kuwapa wapiganaji wake hati za kusafiria.

Hali ya kisheria ya kundi hilo haijulikani: kwa upande mmoja, sheria za Russia zinakataza waziwazi kuwapo kwa makundi haramu ya silaha na makundi ya mamluki nchini humo. Lakini Serikali hiyohiyo haipigi marufuku kundi hilo wala kuwashtaki au kuwakamata viongozi wake.

Viktor Ozerov, mwanasiasa wa Russia na ofisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Shirikisho la Ulinzi na Usalama, wakati mmoja aligusia kwamba marufuku hii haitumiki kwa kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi na katika hali hiyo, Russia haiwajibiki kisheria kwa chochote kuhusu kundi hilo.

Hali hii isiyoeleweka ilitafsiriwa kama zana inayowezesha Serikali ya Russia kuruhusu kwa hiari kampuni binafsi za kijeshi (PMC) inazohitaji, huku ikizuia kuundwa nyingine yoyote ambayo inaweza kuleta hatari kwa Putin na wakati huohuo kudhibiti ukanushaji unaokubalika kwa matendo yao.

Idadi kubwa ya wapiganaji wa kundi hili wamefanya kazi nchini humo, na Aprili 2012 Vladimir Putin wakati huo akiwa waziri mkuu, akilihutubia Bunge la nchi hiyo aliidhinisha wazo la kuanzisha kampuni binafsi za kijeshi nchini humo.Wachambuzi kadhaa wa masuala ya kijeshi wamelitaja kundi la Wagner kama kampuni ya kijeshi ya mtu binafsi ambayo inalipa jeshi la Russia faida kwa kufanya operesheni za kijeshi nje ya nchi hiyo.

Hata hivyo, wapiganaji wa Wagner wametajwa kuwa askari hewa, kutokana na Serikali ya Russia kutowatambua rasmi.

Machi 2017 kundi hilo liliripotiwa katika vyombo vya habari likitajwa kama kundi la wanamgambo linalofadhiliwa na Wizara ya Ulinzi ya Russia.

Septemba 2017, mkuu wa Huduma ya Usalama ya Ukraine (SBU), Vasyl Hrytsak alisema kwa maoni yao, Wagner ni jeshi binafsi la Putin. Alisema SBU ilikuwa ikifanya kazi ya kuwatambua wanachama wa Wagner na kuiweka habari yao hadharani ili washirika wao huko Ulaya wawajue. Kundi la Wagner pia limelinganishwa na Academi, kampuni ya usalama ya Marekani ambayo zamani ilijulikana kama Blackwater.

Kwa mujibu wa SBU, mwaka 2018 wanamgambo wa Wagner walipewa pasi za kusafiria za kimataifa kwa wingi na Serikali ya Russia kupitia ofisi kuu ya uhamiaji.

Madai hayo yalithibitishwa na kikundi cha Bellingcat cha uandishi wa habari za uchunguzi chenye makao yake nchini Uholanzi.

Katika mahojiano Desemba 2018, Putin alisema kuhusu uendeshaji wa Wagner PMC nchini Ukraine, Syria na kwingineko kuwa kila mtu anapaswa kubaki ndani ya mfumo wa kisheria. Na ikiwa kundi hilo linakiuka sheria, ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Russia inapaswa kutoa tathmini ya kisheria .

Lakini, kulingana na Putin, ikiwa hawakukiuka sheria ya Russia, walikuwa na haki ya kufanya kazi na kukuza masilahi yao ya biashara nje ya nchi. Putin pia alikanusha madai kuwa Yevgeny Prigozhin amekuwa akiongoza shughuli za Wagner.

Septemba 2022 Prigozhin alikiri rasmi kuanzisha na kusimamia Kundi Wagner, lililoanza kama kikosi cha kijeshi ambacho kuanzia Mei 2014 kilishiriki vita ya Donbass kikiwa bega kwa bega na Russia.

Kampuni binafsi za kijeshi bado ni haramu nchini Russia, lakini kutokana na Wagner kushiriki katika vita vya Ukraine wamehalalishwa kwa kutajwa na Wizara ya Ulinzi na Serikali hiyo kama vikosi vya kujitolea.

Mei 5, mwaka huu, Prigozhin alimlaumu Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Jenerali Valery Gerasimov, kwamba jeshi la Russia lilijeruhi makumi ya maelfu ya wanamgambo wa Wagner, akisema: "Walikuja hapa kama watu wa kujitolea na wanakufa ili uketi kama paka katika ofisi zako za kifahari".

Katika video iliyotolewa na kusambaa kwenye mitandao ya kijamiii Juni 23 mwaka huu, Prigozhin alisema uhalali wa Serikali ya Russia wa kuivamia Ukraine ulitokana na madai ya uongo.

Juni 24 Prigozhin alituhumiwa na Serikali ya Russia kwa kuandaa maasi ya kutumia silaha, baada ya kutishia kushambulia vikosi vya Russia ili kujibu shambulio la anga dhidi ya wanajeshi wake.

Vikosi vya usalama vya Russia vilimshutumu kwa kuanzisha jaribio la mapinduzi, huku akiahidi kufanya maandamano ya haki dhidi ya jeshi la Russia.

Wakati akitangaza kuandamana kutoka Ukraine kuelekea jiji la Russia la Rostov-on-Don, idara ya usalama ya Taifa ya nchi hiyo, FSB ilisema imefungua mashtaka ya jinai dhidi yake na kuamua kumkamata.

Prigozhin alidai kwamba vikosi vya mamluki vya Wagner viliingia Rostov bila upinzani wowote.

Inadaiwa kuwa makubaliano yaliyosimamiwa na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko yalipunguza kasi ya mapinduzi hayo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Prigozhin alipaswa kuondoka Russia kwenda Belarusi, na kesi ya jinai dhidi yake ilipaswa kufutwa. Hakuna hatua za kisheria ambazo zingechukuliwa dhidi ya wanajeshi wake, na wapiganaji wa Wagner walipaswa kutia saini mikataba na Wizara ya Ulinzi.

Je, Prigozhin alikwenda Belarus? Aliondokaje Russia? Mashtaka dhidi yake yalifutwa? Nini kiliendelea? Usipitwe kesho.