Ujio wa Papa waleta matumaini Sudan Kusini

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wakati Papa akitarajiwa kutembelea taifa la Sudan Kusini hivi karibuni, baadhi ya wananchi nchini humo wanaamini huenda ziara hiyo ikaleta tumaini kurejea kwa amani nchini humo.

Dar es Salaam. Baada ya kukaa karibu muongo mmoja katika kambi ya waliokimbia makazi yao huko Juba Sudan Kusini, Mayen Galuak anatumaini kuwa ziara ya Papa Francis katika mji mkuu wiki ijayo itawatia moyo viongozi wa kisiasa katika kurejesha amani na kumpa nafasi ya kurudi nyumbani.

Kwa mujibu wa Reuters, Galuak mwenye umri wa miaka 44 aliingia katika kambi ya Umoja wa Mataifa, kilomita chache tu kutoka makazi yake, kutafuta usalama siku tatu baada ya mzozo kuzuka mwaka 2013.

Katika miaka iliyofuata, ameshuhudia viongozi wa Sudan Kusini wakitengeneza mikataba ya amani na kuivunja. Ameshuhudia jinsi wanamgambo walivyotekeleza mauaji ya kikabila na migogoro ya nchi hiyo ilivyopelekea njaa.

Papa Francis anatazamiwa kwenda Kongo kuanzia Januari 31 hadi Februari 3 na kisha kukaa siku mbili Sudan Kusini.

Papa amekuwa akitaka kutembelea Sudan Kusini yenye waumini wengi wa Kikristo kwa miaka mingi lakini mipango imekuwa ikiahirishwa kutokana na kukosekana kwa utulivu huku safari iliyopangwa Juni mwaka jana ilikatishwa kutokana na kuumwa goti.

Mjumbe wa Vatican katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema safari hiyo itawakumbusha walimwengu kutopuuza mizozo iliyodumu kwa miongo kadhaa.

"Tuko katika hali mbaya tangu 2013, hatujaona amani," alisema Galuak, ambaye anadai hawezi kusafiri hadi nyumbani kwake alikozaliwa kaskazini mwa nchi hiyo kwa sababu ya hatari ya kushambuliwa ambapo mapigano ya hapa na pale yanaendelea.

Sudan Kusini ilipata uhuru wake mwaka wa 2011. Miaka miwili baadaye mzozo ulizuka wakati majeshi yanayomtii Rais Salva Kiir yalipopambana na yale yanayomtii Makamu wa Rais Riek Machar, ambaye anatoka katika kabila hasimu. Umwagaji damu huo ulizidisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoua watu 400,000.

Mkataba wa amani wa mwaka 2018 ulisimamisha mapigano, lakini baadhi ya makubaliano pamoja na kutumwa kwa jeshi la kitaifa, bado hakuna utekelezaji.

Galuak na watu wengine wengi waliokimbia makazi yao wanasema hawatajisikia salama mpaka vikosi vya umoja vitakapotumwa.
"Kama kungekuwa na amani, tungerejea majumbani mwetu," alisema Nyalon Gatfan, mama wa watoto wanne katika kambi ya Juba.
Galuak na raia wengine 52,000 wanaoishi katika kambi hiyo wanatumaini ya kwamba ziara ya kwanza kabisa ya papa itasababisha viongozi kuheshimu makubaliano yao.

Kuna wakimbizi wa ndani milioni 2.2 nchini Sudan Kusini na wengine milioni 2.3 wamekimbia nchi kama wakimbizi, kulingana na UN.
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, maisha katika kambini yamekuwa magumu. Mwezi Juni, Umoja wa Mataifa ulikata msaada wa chakula kwa Sudan Kusini kwa sababu ya ufadhili wa kutosha.

"Siku hizi, tunakula mara moja kwa siku," Gatfan alisema.
Migogoro, misukosuko ya hali ya hewa na mzozo wa kiuchumi vinaitumbukiza nchi katika uhaba wa chakula. Umoja wa Mataifa ulisema watu milioni 7.76 ambao ni karibu theluthi mbili ya Sudan Kusini wana uwezekano wa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu.

“Nataka Papa awaambie viongozi wetu waelewe mateso tunayopitia,” alisema Gatfan.