Ukraine yalipua ndege za jeshi la Russia

Picha hii iliyopigwa Aprili 4, 2024 gari la dharura lililoharibika kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani huko Kharkiv, Ukraine katika mzozo unaoendelea kati ya nchi hiyo na Russia. Mashambulizi ya anga ya Russia usiku wa kuamkia jana yamejibiwa na mengine yaliyofanywa na Ukraine usiku wa kuamkia leo.
Picha na AFP

Muktasari:

  • Katika shambulio hilo, Ukraine imeteketeza ndege sita na kuharibu nyingine nane katika kambi ya jesdhi la anga iliyopo eneo la Rostov, chanzo cha usalama mjini Kyiv kimeiambia AFP.

Moscow, Urusi/AFP.  Ukraine imefyatua makumi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la kusini mwa Russia la Rostov, ambayo ni makao ya makao makuu ya jeshi lake, ikiwa ni shambulio la kijeshi, mapema leo Ijumaa, maafisa wa Russia walisema.

Katika shambulio hilo, Ukraine imeteketeza ndege sita na kuharibu nyingine nane katika kambi ya jesdhi la anga iliyopo eneo la Rostov, chanzo cha usalama mjini Kyiv kimeiambia AFP.

Kikosi cha Usalama cha SBU cha Ukraine na wanajeshi wameshambulia Uwanja wa Ndege wa Morozovsk, chanzo hicho kimesema na kuongeza "takriban ndege sita za kijeshi za Russia zimeteketezwa na nyingine nane kuharibiwa".
Kufuatia shambulio hilo, Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema imedungua ndege 53 za Ukraine zisizo na rubani usiku wa kuamkia leo,  44 katika eneo la Rostov, huku gavana wa eneo hilo akisema kituo cha umeme kimeharibiwa katika shambulio hilo.
Rostov-on-Don, mji mkuu wa mkoa uliopo karibu na mpaka wa Ukraine, ni mgome ya Jeshi la Russia na eneo muhimu kwa shughuli za jeshi hilo.

"Wakati wa usiku na asubuhi ya Aprili 5, Serikali ya Kyiv imejaribu kufanya mashambulizi kadhaa kwa kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zilishindwa," wizara ya ulinzi imesema.

Mashambulizi mengine ya ndege zisizo na rubani yalilenga maeneo ya mpaka ya Belgorod na Kursk, pamoja na Saratov na Krasnodar.

Huko Saratov, gavana huyo amesema ndege isiyo na rubani ililenga eneo la Engels, jiji lililo karibu kilomita 500 kutoka mpaka ambao ni ngome kuu ya jeshi la anga la Russia, ambayo ilishambuliwa hapo awali.

Wakati huohuo, jeshi la anga la Ukraine limesema Russia imerusha makombora matano na ndege zisizo na rubani 13 katika eneo lake usiku wa kuamkia leo.

Imesema imefanikiwa kuziangusha ndege hizo 13, lakini haikusema lolote kuhusu makombora hayo, ambayo yalilenga eneo la kaskazini mashariki mwa Kharkiv.

Mamlaka zilizowekwa na Russia katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na wanajeshi wa Moscow, pia ziliripoti mashambulizi ya Ukraine siku ya Ijumaa.

Watu watano wamejeruhiwa, wawili vibaya, katika shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye sehemu inayodhibitiwa na Russia ya eneo la Kherson Kusini, huku watu saba wakijeruhiwa katika shambulio la Gorlivka, katika eneo la mashariki la Donetsk, maofisa walioteuliwa na Moscow wamesema.