Upinzani waandamana kupinga matokeo Uchaguzi

Atiku Abubakar (aliyevaa miwani na Kofia) akiwa katika maandamano na wafuasi wake kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu Nigeria.

Muktasari:

  • Atiku Abubakar ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa Februari 25 nchini Nigeria amefanya maandamano pamoja na wafuasi wa chama chake kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Abuja. Kiongozi wa upinzani nchini Nigeria Atiku Abubakar ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais uliofanyika Februari 25, amefanya maandamano na wafuasi wake kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Peter Obi wa Chama cha Labour, ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo, pia amekataa matokeo hayo, na kusema anaenda mahakamani kuwathibitishia Wanigeria kwamba alishinda kinyang'anyiro cha urais

Baraza la uchaguzi wiki iliyopita lilimtangaza Bola Tinubu wa chama tawala cha All Progressive Congress (APC) kama mshindi kuchukua nafasi ya Rais Muhammadu Buhari mwezi Mei.

Takriban watu milioni 25 walipiga kura katika kura ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya Amani, lakini iliyokumbwa na ucheleweshaji wa muda mrefu na hitilafu za kiufundi, hali iliyowakasirisha wapigakura na vyama vya upinzani ambavyo vimedai wizi mkubwa wa kura ulifanyika.

Wafuasi wa Abubakar na wanachama wa chama chake cha Peoples Democratic Party (PDP) wakiwa wamevalia nguo nyeusi kuelekea makao makuu ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) mjini Abuja na kuwasilisha ombi, wakidai udanganyifu katika uchaguzi huo jana Jumatatu.

"INEC inahusika moja kwa moja katika kusaidia wizi mkubwa na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi kwa ajili ya chama tawala," amesema Iyorchia Ayu, mwenyekiti wa PDP.

"Kwa kweli ni hali ya kutisha," amesema kiongozi mwingine wa PDP, Baraka Sani, akiwa amezungukwa na waandamanaji wakiwa na mabango yanayosema "Okoa demokrasia yetu" na "INEC ni fisadi".

Tume imekubali matatizo ya kiufundi siku ya kupiga kura lakini inakataa madai ya udanganyifu.

Uchaguzi wa Nigeria mara nyingi umekumbwa na madai ya udanganyifu.

Katika jitihada za kuboresha uwazi, INEC mwaka huu ilianzisha utambulisho wa kibayometriki wa wapigakura kwa mara ya kwanza katika ngazi ya kitaifa.

Matatizo ya teknolojia mpya pia yalisababisha ucheleweshaji mkubwa na foleni, na kuwakatisha tamaa wengine kupiga kura.

Huku wapiga kura waliojiandikisha wakiwa milioni 93.4, waliojitokeza kupiga kura walikuwa zaidi ya asilimia 27.

INEC inatazamiwa kushughulikia baadhi ya maswala yaliyotolewa na vyama na wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa ugavana na mabaraza ya mitaa siku ya Jumamosi.