Urais DRC pasua kichwa, mwingine ajiengua

Muktasari:

  • Idadi ya wagombea Urais wanaoumuunga mkono Moise Katumbi kuelekea uchaguzi mkuu nchini Kongo inazidi kupaa baada ya hapo jana mwingine kujiengua kwenye kinyang’anyiro hicho na kutangaza kuungana na mmiliki huyo wa klabu ya soka ya TP Mazembe.

Dar es Salaam. Baadhi ya wagombea wa kinyang’anyiro cha Urais nchini DRC wamezidi kujiondoa huku wakimuunga mkono mgombea wa upinzani Moise Katumbi zikiwa zimesalia siku 16 kabla ya uchaguzi.

Hapo jana mgombea wa kiti cha Urais Delly Sesanga ametangaza kujiondoa kwenye mbio hizo na kumuunga mkono mfanyabiashara Katumbi.

Inaelezwa hatua hiyo inatajwa kuimarisha umoja wa upinzani katika juhudi za kumng’oa Rais Felix Tshisekedi aliyepo madarakani akitafuta ngwe ya pili.

Waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo na wagombea wengine wawili ambao sio maarufu wameshajiondoa na kumuunga mkono Katumbi.

Uamuzi huo unazidisha joto la kisiasa nchini humo huku Uchaguzi wa Mkuu nchini ukikaribia ambapo Desemba 20 mwaka huu ndiyo siku ya kupiga kura.

Mpaka sasa wagombea 25 wameshajitokeza akiwamo Rais wa sasa Felix Tshisekedi akipambana na mpinzani wake wa karibu, Martin Fayulu ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2018 ilidaiwa alishinda ingawa hakutangazwa mshindi.

Wagombea wengine maarufu ni Moise Katumbi, Waziri Mkuu mstaafu, Dk Denis Mukwege aliyepata tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018 kwa alivyojitolea kufanya kazi na waathiriwa wa unyanyasaji wa ngono.

Pia wapo mawaziri wakuu wa zamani, Adolphe Muzito na Augustin Matata Ponyo (amejitoa), Mbunge Delly Sesanga, mwanaharakati Floribert Anzuluni na Constant Mutamba ambaye yuko karibu na kambi ya Rais mstaafu, Joseph Kabila.

Wamo pia wanawake wawili ambao ni Marie-Josée Ifoku Mputa, aliyekuwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa Desemba 2018 na Joëlle Bile.

Idhaa ya Kiswahili ya radio ya Ujerumani (DW) imesema kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni mwezi uliopita, kulikuwa na wagombea 26 waliokuwa kwenye kinyang'anyiro hicho.


Fomu ya urais bei juu

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wagombea urais wanatakiwa kuonyesha risiti ya malipo ya faranga za Congo milioni 160, sawa na zaidi ya Sh150.3 milioni kama ada zisizorejeshwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI).

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kiasi hicho kimepunguzwa kutoka dola 100,000 sawa na zaidi ya Sh250.5 milioni katika uchaguzi uliopita wa 2018.