Uturuki yaanza kuwajengea walikosa makazi, vifo vyafikia 50,000

Muktasari:

Uturuki imeanza kazi ya ujenzi ya nyumba zilizoharibiwa kutokana na tetemeko lililoikumba nchi hiyo siku za karibuni. Maofisa wa serikali wamesema jana Ijumaa kuwa takribani watu 50,000 wamefariki dunia Uturuki na Syria.

Uturuki imeanza kazi ya ujenzi ya nyumba zilizoharibiwa kutokana na tetemeko lililoikumba nchi hiyo siku za karibuni. Maofisa wa serikali wamesema jana Ijumaa kuwa takribani watu 50,000 wamefariki dunia Uturuki na Syria.

Zaidi ya majengo 160,000 yenye vyumba 520,000 yaliporomoka au kuharibiwa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Februari 6, 2023 ambalo limeleta madhara kwa watu wengi nchini Uturuki na nchi jirani ya Syria.

Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa na Dharura (AFAD) ilitangaza idadi ya vifo nchini Uturuki kutokana na tetemeko la ardhi iliongezeka hadi 44,218 usiku wa Ijumaa.

Idadi ya vifo vilivyotangazwa nchini Syria ni 5,914, huku idadi ya waliofariki dunia katika nchi hizo mbili imeongezeka na kufikia  50,000.

Ikiwa ni miezi kadhaa imebaki kuelekea uchaguzi nchini Uturuki, Rais Tayyip Erdogan ameahidi kujenga upya nyumba ndani ya mwaka mmoja. Baadhi ya majengo ambayo yalikusudiwa kustahimili tetemeko la ardhi, nayo yalibomoka.

"Kwa miradi kadhaa, zabuni na kandarasi zimefanyika. Mchakato unaendelea haraka sana," afisa mmoja alisema, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, akiongeza hakutakuwa na maelewano juu ya usalama.Mamlaka inasema mahema yametumwa kwa wengi ambao hawana makazi, lakini watu wameripoti shida kuzifikia.

"Nina watoto wanane. Tunaishi kwenye hema. Kuna maji juu (ya hema) na ardhi ina unyevunyevu. Tumeomba mahema zaidi lakini hatujapewa," Melek (67) ambaye alikuwa akisubiri kwenye foleni ya kuchukua msaada nje ya shule katika mji wa Hassa.

Shule hiyo ilikuwa ikitumiwa kama kituo cha kusambaza misaada na kikundi cha watu waliojitolea kiitwacho Interrail Uturuki. Mkazi mwingine wa eneo hilo, Sumeyye Karabocek, alisema uhaba wa mahema umekuwa tatizo kubwa zaidi.