Uwekezaji wa China nchini Kenya

Muktasari:

Serikali ya Kenya imetoa kandarasi tatu ambazo hazikutarajiwa za ujenzi wa reli, treni ya abiria na huduma ya mizigo zilizofadhiliwa,  kusanifiwa na kujengwa na China.

Serikali ya Kenya imetoa kandarasi tatu ambazo hazikutarajiwa za ujenzi wa reli, treni ya abiria na huduma ya mizigo zilizofadhiliwa,  kusanifiwa na kujengwa na China.

Wataalamu kutoka China na Afrika wamesema suala hilo lililoibuliwa halikuwahi kujulikana awali kutokana na usiri unaozunguka mikataba ya mikopo ya China.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kutokana na China kuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Kenya, nchi hiyo ya Kiafrika sasa inadaiwa na China deni kubwa.


"Taasisi za kifedha za China zinatoa msaada wa kifedha kwa ushirikiano kati ya China na Kenya kwa mujibu wa kanuni za kibiashara na soko zinazokubalika kimataifa, ambazo zilipunguza ukosefu wa fedha wa Kenya na kuongeza uwezo wa Kenya wa kujiletea maendeleo huru," msemaji wa Wizara ya China amesema na kukaririwa na New York Times.

Benki za China  ziliipiga Kenya faini ya shilingi bilioni 1.312 za Kenya katika mwaka uliomalizika Juni mwaka huu kwa kutolipa mikopo iliyotolewa kujenga reli ya kisasa (SGR).

Kenya ilichukua  zaidi ya shilingi nusu trilioni kutoka kwa wakopeshaji wa China, wakiongozwa na Benki ya Export-Import ya China, kufadhili ujenzi wa SGR kutoka Mombasa hadi Naivasha.

China ilichangia takriban theluthi moja ya gharama za huduma ya deni la nje la Kenya mwaka 2021-22, ndio mkopeshaji mkuu baada ya Benki ya Dunia.

Kenya ilitumia jumla ya Sh117.7 bilioni kulipia deni la China katika kipindi hicho, ambapo takriban Sh24.7 bilioni ni malipo ya riba na karibu Sh93 bilioni katika ukombozi, kulingana na hati za bajeti.

Mkataba wa kufadhili awamu ya kwanza ya SGR, mradi mkubwa zaidi wa miundombinu nchini Kenya kwa gharama tangu uhuru, ulishuhudia China ikiipiku Japan kama mkopeshaji mkuu zaidi wa Kenya.

Deni la Kenya liliongezeka zaidi ya mara nne hadi Sh8.58 trilioni chini ya utawala wa rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.