Venezuela yadai kubaini waliotaka kumuua Maduro
Muktasari:
- Uchunguzi unaofanywa ukiwahusisha waendesha mashtaka wanne, umefanikisha kubaini maeneo ambayo ndege hizo zilirushwa pamoja na kuwatia mbaroni marubani wawili wa drone, mwanasheria huyo mkuu alisema Jumatatu.
Caracas, Venezuela. Mamlaka za Venezuela zimesema zimefanikiwa kutambua waliopanga njama za jaribio la kumuua kwa ndege isiyo na rubani, drone, Rais Nicolas Maduro pamoja na watu waliosaidia, alisema Mwanasheria Mkuu Tarek William Saab.
Uchunguzi unaofanywa ukiwahusisha waendesha mashtaka wanne, umefanikisha kubaini maeneo ambayo ndege hizo zilirushwa pamoja na kuwatia mbaroni marubani wawili wa drone, mwanasheria huyo mkuu alisema Jumatatu.
"Tunafahamu pia maeneo ambako ndege hizo zilikuwa zimewekwa katika siku za kuelekea kufanya shambulio. Tumewatambua watu waliotengeneza vilipuzi na walioandaa silaha na mafungamano yao kimataifa,” alisema Saab.
Vilevile, alisema hicho kinachoitwa jaribio la mauaji ni "usaliti kwa nchi hii mama, ni jaribio la mauaji ya watu, ugaidi, na kula njama za kutenda uhalifu na kufadhili ugaidi."
Taarifa hiyo ya Saab imekuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Néstor Reverol kusema watu sita walikuwa wamekamatwa wakihusishwa na tukio la shambulio lililofanyika Jumamosi jijini Caracas.
Watuhumiwa hao walishtakiwa kwa makosa ya “ugaidi na kula njama”, Reverol alisema, na kwamba mmoja wao ilikuwepo hati ya kumkamata akituhumiwa kuhusika na shambulizi lililofanyika Agosti 2017 kwenye kambi ya jeshi Valencia. Mwingine aliwahi kukamatwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali mwaka 2014.
Maduro alinusurika kuuawa wakati ndege aina ya drone zikiwa zimebeba vilipuzi zilipopiga karibu na eneo alilosimama wakati akihutubia gwaride la wanajeshi walipokuwa wakifanya maadhimisho ya miaka 81 ya jeshi hilo.
Baada ya kuokolelewa, Maduro Jumapili alilihutubia taifa kwa njia ya televisheni ambapo alimshutumu Rais wa Colombia Juan Manuel Santos na watu wenye mrengo wa kulia aliodai wako Marekani.