Vifo tetemeko la ardhi vyafikia 25,000 Uturuki, Syria

Muktasari:

  • Hali ya huzuni na simanzi yaendelea nchini Uturuki na Syria hii ni baada ya kuthibitika kutokea kwa vifo zaidi ya watu 25,000, vilivyotokana na tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu ya Februari 6, kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria. 

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 25,000 sasa wamethibitika kufariki baada ya tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu ya Februari 6, kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria.

Kwa mujibu wa kituo cha habari ‘BBC’ wameeleza kwamba msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameiambia BBC sasa ni wakati wa kuweka siasa zote pembeni na kupeleka misaada Syria.

Mwandishi wa BBC, Quentin Sommerville aliyepo Syria, ameeleza kwamba watu wamemuambia kuwa wamechelewa kupata msaada.

Wakati huohuo, mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths, ambaye yuko Uturuki, ameelezea tetemeko la ardhi la Jumatatu kama tukio baya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mia moja katika eneo hilo.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameripotiwa kuwasili katika mji uliokumbwa na tetemeko la ardhi wa Aleppo leo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, ambapo amesema, "Tumeleta tani 35 za vifaa muhimu vya matibabu vinavyohitajika kushughulikia mahitaji ya wale waliojeruhiwa na tetemeko la ardhi.”

Katika kutekeleza misaada mbalimbali kivuko cha mpaka kati ya Armenia na Uturuki kimefunguliwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 35 ili kuruhusu msaada mbalimbali.

Serdar Kilic, mjumbe maalum wa Uturuki kwa mazungumzo na Armenia, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii ‘Twitter’ kwamba lori tano za msaada zikiwemo dawa, chakula na maji ziliwasili Uturuki kutoka kwenye mpaka wa Alican asubuhi ya leo.

Shirika la habari la serikali lilisema hii ni mara ya kwanza kufunguliwa kwa mpaka huo tangu 1988.