Wahamiaji 6,000 wapoteza maisha wakijaribu kuingia Ulaya

Muktasari:

  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema takribani watu 186,000 wamewasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterania mwaka 2023. Katika kipindi hicho watu  60,000 walipoteza maisha wakijaribu kuingia Hispania.

Dar es Salaam. Vijana wenye ndoto za kuzamia Ulaya mmesikia hii? Wahamiaji 6,618 walikufa au kupotea baharini wakijaribu kuingia Hispania kupitia njia ya bahari, kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wahamiaji nchini Hispania.

Vijana kutoka mataifa mengi ya Afrika wamekuwa wakitamani kwenda Ulaya kutafuta maisha mazuri, hata hivyo wengi wamekuwa wakipoteza maisha wakati wakijaribu kuvuka bahari kuingia huko.

Hali hiyo inaonekana kutishia usalama kwa wale wanaotaka kutumia njia za panya, hivyo, kijana unatakiwa kutafakari mara mbili kabla ya kuchukua hatua hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya jana ya shirika la kutetea haki za wahamiaji nchini Hispania, mwaka 2023, wahamiaji 6,618 walikufa au kupotea habarini wakijaribu kuingia Hispania kupitia njia ya bahari.

Maeneo ya Hispania ya Ceuta na Melilla yanayozungukwa na na eneo la Afrika Magharibi, yamekuwa kivutio kikubwa cha wahamiaji Waafrika wanaojaribu kuingia Ulaya.

“Idadi hiyo ni takribani mara tatu zaidi ya iliyorekodiwa mwaka 2022, ambapo wahamiaji 2,390 walipoteza maisha,” inaeleza taarifa ya shirika hilo.

Wakati tishio hilo likiongezeka Hispania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limesema takribani watu 186,000 waliwasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterania mwaka 2023. 

Kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR, watu 130,000 wamesajili nchini Italia idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.