Wanafunzi wamshambulia mwalimu mkuu kwa kugoma kuhama

Walimu hao wa Shule ya Sekondari ya Kibaale, iliyoko katika Wilaya ya Namutumba nchini Uganda wanadaiwa kuwachochea wanafunzi ili kumpiga mwalimu mkuu wa shule hiyo na tayari Jeshi la Polisi linawashikilia kwa mahojiano.

Walimu hao wapatao wanne wa Shule ya Sekondari Kibaale wanashikiliwa na Jeshi la Polisi la nchini Uganda kwa makosa ya kuwachochea wanafunzi kumpiga mwalimu mkuu wa shule hiyo, Kagoye Samanya.

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Namutumba (DPC), Hebert Nuwagaba amesema tukio hilo limetokea Machi 28 ambapo walimu hao ambao hakutaja majina yao wapo chini ya ulinzi wakitoa taarifa za tuhuma za kuwasaidia wanafunzi kugoma na kumpiga Mwalimu Mkuu, Samanya.

"Tumewaweka chini ya ulinzi huku uchunguzi wetu ukiendelea," amesema Nuwabaga na kuongeza kuwa pia wanamshikilia kiongozi wa wanafunzi anayedaiwa pia kuongoza wenzie kutoka madarasani na kuanza kumpiga Samanya.

Inadaiwa Samanya alikumbwa na masahibu hayo baada ya kukataa uhamisho wake wa kwenda katika shule nyingine ya sekondari iitwayo Kibuku.

Tovuti ya Monitor ya nchini humo imeripoti kwamba tangu kuanza kwa muhula wa masomo katika shule hiyo yenye wanafunzi wapatao 500 imekuwa ikiendeshwa na walimu wakuu wawili, ambao ni Stephen Mutono na Kagoye Samanya.

Inasemekana Mutono aliripoti Februari 6 na kusaini kama mwalimu mkuu mpya, lakini hata hivyo anaulaumu uongozi wa wilaya kwa madai ya kumzuia kuingia ofisini huku ikiripotiwa kumuunga mkono Samanya.

Thomas Matende, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Namutumba (RDC), alisema jambo hilo halihitajiki katika wakati ambao shule hiyo inamgogoro wa nani mwalimu mkuu wa kweli.

“Tunapendekeza walimu waendelee kufundisha na kuiacha Wizara ya Elimu ifanye kazi yake. Wizara inafahamu kinachoendelea katika Shule hii,” amesema.

Imeandaliwa na Sute Kamwelwe