Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi awasili Afrika Kusini

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amewasili nchini Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi ya kuandaa mkutano kati ya nchi hiyo na mataifa ya Afrika.

Pretoria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amewasili nchini Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi ikiwa pamoja na maandalizi ya mkutano kati ya nchi hiyo na mataifa ya Afrika.

Ziara hiyo inakuja wakati Russia ikiendelea na vita kati yake nan chi ya Ukraine inayoungwa mkono Marekani na baadhi ya Mataifa ya Ulaya.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Russia (TASS) Lavrov amewasili nchini humo leo Jumatatu Januari 23 katika kituo cha jeshi la anga la Afrika Kusini Waterkloof.

Anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Naledi Pandor katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria.

Mawaziri hao wana uwezekano mkubwa wa kujadili matayarisho ya mkutano wa pili wa kilele kati ya Russia na Afrika unaotazamiwa kufanyika Julai 26-29 katika mji wa St. Petersburg nchini Russia.

Lavrov na mwenzake wa Afrika Kusini walikutana mara ya mwisho kwenye kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ambapo walisisitiza maslahi ya pande zote mbili katika kuimarisha mazungumzo ya kisiasa na maendeleo zaidi ya mahusiano ya ushirikiano wa kimkakati.