Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

34 wakutwa na matatizo ya moyo Kagera

Muktasari:

Madaktari bingwa kutoka JKCI wameweka kambi ya uchunguzi ya siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba.

Kagera. Watu 34 kati ya 194 waliofanyiwa uchunguzi kwenye kambi maalumu ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Kagera sawa na asilimia 17 wamekutwa na matatizo ya moyo.

Takwimu hizo zimetolewa Machi 21, 2024 na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI, Dk Yona Gandye.

Kambi ya uchunguzi ya siku tano inafanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba mkoani Kagera, imeanza Machi 18, 2024.

Dk Gandye amesema waliobainika kuwa na tatizo la moyo lililofikia hatua mbaya, wamepatiwa rufaa ya kwenda kupatiwa huduma za kibingwa JKCI mkoani Dar es Salaam.

Awali, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka JKCI, Dk Nuru Letara ametaja baadhi ya tabia zinazochangia watoto kuugua magonjwa ya moyo, ikiwemo mjamzito kutomeza dawa za foliki asidi ipasavyo, uvutaji sigara na unywaji wa pombe.

"Nikitolea mfano katika Taasisi ya JKCI pekee tunapokea watoto 30 hadi 40 kwa siku wenye matatizo ya moyo, na watoto zaidi ya 300 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji hospitalini hapo," amesema Dk Letara.


Amewataka wazazi kuweka mipango kabla ya kushika ujauzito ili kuhakikisha mtoto anayezaliwa anakuwa na afya njema.

Dk Letara amesema mtoto mwenye afya ni matokeo ya maandalizi mazuri ya wazazi.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake amesema uwepo wa kambi ya madaktari hao, utapunguza gharama kwa wananchi wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya matibabu ya moyo ya kibingwa katika Hospitali ya Bugando na JKCI.

Mwassa amesema;: "Shinikizo la damu lilikuwa likiongoza kwa idadi ya wagonjwa waliokuwa wakitibiwa katika hospitali ya Bukoba. Wagonjwa wa nje walikuwa asilimia 7.92, na wa ndani walikuwa 5.58 kati ya wagonjwa waliokuwa wanalazwa Hospitali ya Bukoba."

Mkazi wa Kata ya Nshambya, Manispaa ya Bukoba, Anajoyce Ngilwa mbali na kushukuru Serikali kwa kupeleka madaktari hao, amesema kupitia kambi hiyo wataweza kubaini changamoto za kiafya zinazowatesa.