ACT-Wazalendo ilivyopanga safu yake kuelekea uchaguzi wa 2020

Zilikuwa wiki mbili za mshikemshike, mtikisiko na mabadiliko ndani ya chama ya ACT- Wazalendo ambacho juzi kilikamilisha rasmi safu ya viongozi wa juu wa chama hicho wanaotazamiwa kuipeleka mbele kwa miaka mingine mitano.

Chama hicho kilifanya mkutano wake wa pili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014 uliokuwa na ajenda kuwachagua viongozi mbalimbali wa juu ambao ni kiongozi wa chama, mwenyekiti na makamu wake wawili, wa Tanzania Bara na wa Zanzibar.

Mkutano mkuu wa kwanza wa chama hicho ulifanyika Machi 28, 2015 ambapo viongozi mbalimbali walichaguliwa. Viongozi hao ni mwenyekiti, makamu wenyeviti bara na visiwani , katibu mkuu wa chama na manaibu wake wawili na kiongozi mkuu wa chama hicho.

Katika mkutano huo, Zitto Kabwe alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama wakati, Anna Mghwira alichaguliwa kuwa mwenyekiti.

Hata hivyo, Mghwira baada ya miaka kadhaa alijiuzulu nafasi hiyo alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa. Pia Mwigamba alichaguliwa kuwa katibu mkuu naye alijiuzulu.

Hadi mkutano wa pili unafanyika kuwachagua viongozi wa juu, ACT-Wazalendo haikuwa na mwenyekiti wala katibu mkuu bali nafasi hizo zilikuwa zikikaimiwa na Dorothy Semu (kaimu katibu mkuu) na Yeremia Maganja (makamu mwenyekiti).

Katika uchaguzi huo uliohitimishwa JUmatatu, Zitto amekuwa miongoni mwa viongozi wachache waliobaki ndani ya chama hicho ambao waliochaguliwa katika uchaguzi wa 2015 na kudumu hadi 2020.

Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu na uchaguzi wa kitaifa kwa ujumla ulianza Januari 27 na kuhitimishwa Machi 16 ikiwa ni sawa na siku 49.

Uchaguzi wa viongozi wakuu ulifanyika Machi 14 hadi 16, 2020 ukitanguliwa na chaguzi nyingine za ngome ya wazee, uliofanyika Machi 10, ngome ya vijana Machi 9 ngome ya wanawake Machi 8.

Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ngazi ya chama hicho taifa ni pamoja na kiongozi wa chama, naibu kiongozi, mwenyekiti wa Taifa, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, katibu mkuu, wajumbe wa halmashauri kuu (nafasi 15) na wajumbe wa kamati kuu (nafasi nane).

Ngome ya wanawake nafasi zinazogombewa ni mwenyekiti wa ngome, makamu mwenyekiti wa ngome, katibu na wajumbe wa halmashauri kuu (nafasi 15) na wajumbe wa kamati kuu (nafasi nane).

Wakati ngome ya vijana nafasi zinazogombewa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, katibu na naibu wake, wajumbe wa halmashauri kuu Taifa na wajumbe wa mkutano mkuu.

Katika uchaguzi huo, Zitto alifanikiwa alitetea nafasi hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kupata kura 276 sawa na asilimia 73.6 dhidi ya mpinzani wake, Ismail Jussa aliyepata kura 91 sawa na asilimia 24.2.

Kwa upande wake, Maalim Seif aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alipata kura 337 sawa asilimia 93.30 dhidi ya Nyangaki Shilungushela aliyepata kura nane na Maganja kura 20 sawa na asilimia 5.55.

Wajumbe wa mkutano huo pia walimchagua Dorothy kuwa makamu mwenyekiti Bara akiwashinda Mary Mongi, Edgar Mkosamali na Juma Mkumbi. Upande Zanzibar aliyeshinda nafasi hiyo ni Juma Duni Haji ambaye aliyekuwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo.

Safu hiyo ya viongozi wa juu ilikamilishwa kwa Halmashauri Kuu ya ACT- Wazalendo yenye wajumbe 75 kumchagua Ado Shaibu kuwa katibu mkuu wa pili wa chama hicho kwa kura zote sawa na asilimia 100.

Hii ilikuwa baada ya aliyekuwa mshindani wake, Joran Bashange kuandika barua ya kujitoa dakika za mwisho, na baadaye akateuliwa kuwa naibu katibu mkuu Bara na mwenzake wa Zanzibar aliteuliwa Ahmed Mazrui.

Kijana mwanaharakati Abdul Nondo, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ngome ya vijana, mbunge wa zamani wa viti maalumu Mkiwa Kimwanga alishinda nafasi ya uenyekiti wa ngome ya wanawake na Yassin Mohamed akiibuka mshindi wa uenyekiti wa ngome ya wazee wa chama hicho.

Chaguzi za ngome za chama hicho, zilikuwa zenye msisimko na ushindani mkubwa kwa sababu zilirudiwa mara tatu hasa nafasi ya uenyekiti baada ya wagombea waliojitokeza kushindwa kufikisha asimilia 50 kwa mujibu kanuni za uchaguzi wa ACT-Wazalendo.

Licha ya mchakato huu kukakamilika na safu ya viongozi wa kupatikana lakini chama hicho kimeweka historia ya kipekee kwa kuendesha mdahalo kwa wagombea wake wa ngazi ya uenyekiti na kiongozi wa chama hicho na ngome zake.

ACT-Wazalendo kimekuwa chama cha kwanza kwa wagombea wa nafasi hiyo walipata kujieleza sababu za wao kugombea kisha kuulizwa maswali na washiriki wa mdahalo wakiwamo wanahabari.

Katika mdahalo huo, weanachama hao kila mmoja kwa wakati wake alijitahidi kufafanua jinsi atakavyokiongoza chama hicho kwa ufanisi, bila kujali mazingira yaliyopo nchini kisiasa. Kwa ujumla wengi waliojinadiwalijigamba kukiletea ushindi chama hicho katika uchaguzi ujao

Wasemavyo wanachama

Wanachama wa chama hicho wanasema mdahalo umewapa fursa ya kuwapima na kujua uwezo wa wagombea wao ambao asilimia kubwa waliibuka kidedea katika uchaguzi huo.

“Mdahalo mzuri sana wapiga kura walipata fursa ya kuwachuja wagombea wanaowahitaji. Mdahalo huu ulitupa fursa ya kujua nani tumempigia kura ili akisaidie chama hiki kwa siku za usoni hasa kwenye uchaguzi mkuu,” anasema Makiyye Juma Ali.

Makiyye anasema safu ya viongozi wa juu waliopatikana italeta msisimko katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, na hiyo itakuwa sindano kwa vyama vingine vyama.

Anasema uchaguzi huo umeendeshwa kidemokrasia, uwazi na kila mwanachama mwenye uwezo amepata nafasi ya kushiriki kikamilifu mchakato kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.

“Suala la ushiriki wa wanawake limezingatiwa katika uchaguzi huu pamoja na vijana kupata fursa ya kuwa viongozi wa ACT- Wazalendo na waliochaguliwa ni wazoefu kwenye siasa na watakuwa na hamu kujua nini watakifanya hasa kwenye uchaguzi mkuu.

“Watanzania na wafuatiliaji wa siasa watakuwa na shauku kujua nini kitatokea kwa chama hiki, kwa sasa mmoja wa viongozi alikuwa chama kingine kabla ya kuhamia chama cha sasa na kuwa mwenyekiti,” anasema Makkiye.

Wakati Makkiye akieleza hayo, mwanachama mwingine Veronica Martin anasema mdahalo huo umekijenga chama hicho na umeweka msingi bora kwa siku za baadaye. Akizungumzia safu ya viongozi wa juu waliopatikana, Veronica anasema watakuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto za wananchi kwa sababu watawachagua wawakilishi sahihi watakaokwenda kupigania maslahi yao.

Naye, Mohamed Mtutuma anasema viongozi waliochaguliwa ni makini wenye busara na ana matumaini makubwa chama hicho kitafikia malengo na mikakati mbalimbali waliyopanga.

“Viongozi hawa wanajua uchungu wa chama hawawezi kutusaliti au kusajiliwa kwenda chama kingine. Ni watu makini wenye uelewa wataifikisha mbali taasisi hii,” anasema Mtutuma.

Kwa upande wake, Mkumbi anasema uchaguzi wa chama hicho ulitawaliwa na uwazi, haki na demokrasia na kila mtu mwanachama ambaye si mjumbe alipata fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa ACT-Wazalendo.

“Safu ya viongozi waliopatikana ni ya ushindi mkubwa kwa chama hiki kwa sababu watu makini na bora. Viongozi hawa tuliowachagua hawanunuliki, hawana bei ni watu wenye imani na wanajua umuhimu wa chama,” anasema Mkumbi.

Akizungumzia mdahalo huo, Mkumbi anasema umeleta funzo kwa wagombea sambamba na kuwapima na uliwapa fursa ya wanachama kujua aina ya mtu wanayetakkumchagua ili awe kiongozi wa ACT-Wazalendo kwa miaka mitano ijayo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama hicho, Zitto alisema endapo chama hicho kikishika dola katika uchaguzi wa mwakani kitahakikisha kinaijenga Tanzania inayopaa kiuchumi kwa kubuni na kutekeleza sera za uchumi shirikishi utakaozalisha ajira.

Alichokisema Zitto

Zitto alisema ACT Wazalendo itahakikisha inavutia uwekezaji wa nje ili kuongeza mitaji nchini na kupanua shughuli za uzalishaji mali pindi chama hicho kikifanikiwa kuingia madarakani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

“Ni muhimu wananchi kufahamu tutapokea uongozi wa nchi wenye changamoto lukuki zinazotokana na muundo wetu na idadi ya watu. Najua changamoto hizi nyingine zinatokana na chama kilichopo madarakani,” anasema.

Akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa Zitto anasema, “sina maneno mengi ya kueleza ndani ya miaka mitano iliyopita chama hiki kilionekana hakitainuka. Lakini tumefanya mkutano wa kihistoria na kutoa funzo kwa vyama vingine.” “Nimeomba miaka mingine mitano nashukuru wajumbe kwa imani yenu kwangu kuendelea kuifanya kazi hii. Sioni kama mmenipa mzigo bali ni nafasi adimu hasa kwa wakati huu,” alisema Zitto.

Anasema ACT- Wazalendo ni chama kimoja na hakuna nyufa zitakazopita ili kigawanyike na uchaguzi huo wa kihistoria ni ishara tosha, akisema kwamba wamepeleka salamu kwa mahasimu wao na kazi iliyobaki ni kuhakikisha wabunge wanapatikana wengi sambamba na kushika dola Tanzania bara na Zanzibar.

Maalim Seif aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar anawashukuru wajumbe hao kwa imani yao ya kumchagua kushika nafasi hiyo akiwaahidi kutowaangusha katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Mmenichagua kwa matumaini sitowaangusha nitashirikiana na viongozi wenzangu na wanachama kukiimarisha na kukijenga chama hiki kwa ajili uchaguzi ujao. Nawapongeza wote waliojitokeza kushiriki, mimi sio mshindi wala walioshindwa sio washindi, mshindi ni ACT-Wazalendo,” anasema Maalim Seif.

Katika mkutano huo, chama hicho kilifanya mabadiliko ya katiba yao baada ya Sheria ya Vyama vya Siasa kufanyiwa marekebisho na jumla ya mapendekezo 18 ikiwamo ya nafasi ya bodi ya wadhamini na mfumo wa upigaji kura yaliwasilishwa na kupitishwa na wajumbe wa mkutano huo.