Ajira Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zatangazwa

Muktasari:

  • Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lawaita katika ajira waliohitimu JKT na walioko katika kambi mbalimbali kuomba mchakato huo kabla ya Disemba 8, 2022.

Dar es Salaam. Vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na walioko katika makambi mbalimbali wanatajarajiwa kunufaika na ajira baada ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutangaza nafasi za mchakato huo.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo, leo Alhamisi Novemba 24, 2022 imetangaza mchakato huo huku ukiainisha sifa na vigezo vinahitajika ili kujiunga na zimamoto na uokoaji.

Miongoni mwa vigezo ni wahitaji wote waliohitimu kidato cha nne kuanzia mwaka 2020 hadi 2021 na wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 23.

Wakati miongoni mwa sifa zinazohitaji ni pamoja na awe raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, ahitimu mafunzo ya JKT au aliyepo kambini, cheti za kuzaliwa, kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho iliyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho (Nida), afya njema ya kimwili na kiakili na asiwe na kumbumbu za uhalifu.

Sifa zingine ni asiwe na alama kuchorewa mwilini ‘tatoo’ asiwe ameoa wala kuolewa, awe tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya zimamoto na uokoaji, awe na urefu usiopungua futi 5.7 kwa mwanaume na futi 5.4 kwa mwanamke.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, mwombaji atatakiwa kutuma maombi yake kwa kuandika barua za maombi kwa mkono akiambatanisha nakala mbalimbali ikiwemo, cheti cha kuzaliwa, fomu ya uthibitisho wa siha nje kutoka mganga wa Serikali, picha tatu za pasipoti nakala ya kitambulisho cha Taifa.

“Nakala za vyeti zithibitishwe na kamishna wa viapo au hakimu na barua zitakazowasilishwa kwa njia ya mkono hazitapokelewa na mwisho wa kupokea maombi ni Disemba 8 mwaka huu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.