Aliyepigwa risasi akosa pesa ya matibabu, ahofia kupoteza mguu

Benjamin Shinda akionyesha sehemu aliyopigwa risasi na mwajiri wake akidai anamwibia, katika kata ya Mtibwa, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Na Mpiga Picha Wetu
Muktasari:
- Maisha ya kijana Benjamin Shinda, aliyepigwa risasi mguuni na mwajiri wake yanaendelea kuwa magumu, baada ya hali ya jeraha lake kuwa mbaya zaidi kwa kukosa huduma za matibabu.
Dar es Salaam. Maisha ya kijana Benjamin Shinda, aliyepigwa risasi mguuni na mwajiri wake yanaendelea kuwa magumu, baada ya hali ya jeraha lake kuwa mbaya zaidi kwa kukosa huduma za matibabu.
Kijana huyo mkazi wa Mtibwa mkoani Morogoro, alipigwa risasi Januari 24, mwaka huu na mwajiri wake akidai amemwibia fedha ya kazi ya kulima vibarua kwa trekta.
Licha ya madai ya wizi yaliyoibuliwa na mwajiri wake hadi kumpiga risasi ya mguuni, Shinda (24), anasema kwa siku nne zote alizofanya kazi kwa trekta hilo, hakukuwa na chochote kilichopatikana kwa kuwa lilikuwa bovu.
“Alinipiga risasi siku nne baada ya kuanza kazi, siku ya kwanza nilikwenda shambani trekta liliharibika, hali ilikuwa hivyo hata kwa siku tatu baadaye.
“Siku hiyo nililirudisha nyumbani lifanyiwe matengenezo makubwa, ndipo nilipopigwa risasi,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi, Shinda alisema hali ya mguu wake imefikia hatua ya kutonyooka kwa kuwa hapati tena huduma za matibabu katika Hospitali ya Bwagala wilayani Mvomero.
“Bwagala ilikuwa hospitali kubwa, pale huduma zao zilikuwa nzuri, lakini kwa sasa sina hela ya kuendelea na matibabu, kwa hiyo nimesitisha huduma katika hospitali hiyo,” alisema.
Kukosekana kwa fedha, alieleza kumesababisha badala ya kwenda hospitali kupata baadhi ya huduma, anakwenda kukisafisha kidonda katika duka la dawa, ambapo hata hivyo hajakisafisha kwa siku nne hadi juzi.
“Sasa hivi kuna duka la dawa nakwenda kuosha hapa karibu na nyumbani, lakini hali imekuwa mbaya zaidi, sina hela ya kuendelea kupata huduma, kwa hiyo hapa leo nina siku nne sijasafisha kidonda,” alisimulia.
Alisema kwa sasa kidonda kimeanza kuwa na rangi ya kijani na hata mguu hauwezi tena kunyooka muda wote anaukunja.
Kutokana na maisha ya udereva wa trekta na magari, Shinda alisema kwa sasa anaishi kwa kuomba fedha kwa marafiki zake ili kupata walau mlo wa siku wa familia yake.
Kijana huyo pamoja na umri mdogo alionao, ndiye anayetegemewa na familia yake yenye wadogo zake watatu, mama na kaka yake.
“Ndugu zangu walikuwa wananitegemea kwenye hizo shughuli zangu za udereva nipate chochote tukamilishe ratiba za hapa nyumbani, lakini hali imekuwa mbaya kwa sasa sina uwezo wa kufanya kazi yoyote,” alisema.
Shinda alisema anahofia kuupoteza mguu wake, ambao anasema ndiyo msingi wa shughuli mbalimbali zinazomuingizia kipato.
“Polisi tunaambiwa wanaendelea na uchunguzi kabla ya kesi kupelekwa mahakamani, mtuhumiwa alikamatwa na sasa ameachiwa kwa dhamana yupo uraiani.
“Sina uhakika kama nitapata haki katika hili, wakati mimi nimo ndani nateseka na mguu huku nikihofia kuupoteza, aliyenifanyia kitendo hiki anaendelea na maisha yake.”
Kwa upande wa mjomba wa Shinda, Emmanuel Siame alisema awali aliyefanya tukio hilo alishiriki kwa kugharimia matibabu ya kijana huyo, lakini baadaye alisitisha.
“Alikuwa anamlipia, sasa hivi halipi tena na tumekosa hela kabisa mguu unamsumbua hatuna namna ya kumpatia matibabu,” alisema.
Kwa mujibu wa Siame, amekwenda kwenye vyombo vya ulinzi na usalama mara kadhaa na anajibiwa kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika ili ipelekwe mahakamani.
Awali gazeti hili liliporipoti tukio la Shinda kwa mara ya kwanza, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia kwa Mkurugenzi wake, Anna Henga alisema kuwa wamelazimika kumtuma mtetezi wa haki za binadamu, aliyeko mkoani Morogoro kufuatilia kwa karibu.