Angel Nyigu: Usiichukulie poa kazi yangu ya kunyonga nyonga mwili

Angel Nyigu: Usiichukulie poa kazi yangu ya kunyonga nyonga mwili

Muktasari:

  • Angel ni msakata dansi maarufu hapa nchini akifanya kazi na wasanii kadhaa, akiwamo Diamond, Zuchu na Harmonize.

Nani alitarajia kukata nyonga kungenitambulisha duniani, pengine wakati ninaanza kila mtu alikuwa ananichukulia nisiyekuwa na chaguo zuri la kazi.

“Lakini nyonga, mikogo, kunyonga nyonga viungo vya mwili kumenitambulisha Afrika nzima na inawezekana duniani pia, naamini bahati yangu haipo mbali, inakuja ninazidi kuongeza bidii,” anasema Angel Nyigu, baada ya kukosa tuzo ya Afrimma.

Angel ni msakata dansi maarufu hapa nchini akifanya kazi na wasanii kadhaa, akiwamo Diamond, Zuchu na Harmonize.

Alitajwa kuwania tuzo za Afrimma kwenye kipengele cha dansa bora Afrika, ambapo bahati ilimwangukia dansa Soweto’s Finest kutoka nchini Afrika Kusini.

Katika kipengele hicho Angel alishindanishwa na Poco Lee (Nigeria), Henry Le Sheriff (Cameroon), La Petite Zota (Ivory Coast), Masaka Kids Africana (Uganda), Sayrah Chips (Nigeria) na Soweto’s Finest (Afrika Kusini).

Angel alifanya mahojiano ya moja kwa moja na gazeti hili kuelezea mafanikio yake na anavyozungumzia ushiriki wake katika tuzo hizo.


Swali: Ilikuwaje uliposikia umetajwa kuwania tuzo za Afrimma?

Angel Nyigu: Kwanza nilichelewa kusikia, nikawa naambiwa na watu, nilijiridhisha kuwa ni kweli nimetajwa kuwania tuzo hizo, haraka niliangalia wasanii ninaoshindana nao, nikasema kimoyomoyo haki kazi ninayofanya ni kubwa.


Swali: Kwa nini ulisema kazi unayofanya ni kubwa?

Angel Nyigu: Nilisema na kuamini hivyo kwa sababu watu niliotajwa kushindanishwa nao wanafanya vitu vikubwa katika jukwaa na kusakata dansi. Kabla hajatangazwa mshindi nilikuwa nina furaha na kujiona ni mshindi na nimeiwakilisha nchi vema.


Swali: Mbona ulijiamini kabla ya kutangazwa mshindi na mwisho wa siku hukupata tuzo?

Angel Nyigu: ...Nani alimini siku moja kupitia kunengua, kuzungusha viungo na nyonga ningetajwa katika tuzo kubwa kama hizo achilia mbali za hapa ndani kama zingekuwepo? Huo kwangu ulikuwa ushindi na niliamini nimefungua dirisha na matumaini mapya kwa wasichana wanaopenda kufanya shughuli kama yangu.


Swali: Kwa nini wasichana?

Angel Nyigu: Kwanza jamii bado haiwapi nafasi wasichana kuonyesha vipaji vyao. Huko ni kwenye muziki, uigizaji na michezo kwa ujumla, sikuambii katika udansa na unenguaji, hivyo kuchaguliwa kwangu kuwania tuzo kubwa za Afrimma, labda kutaonyesha ni kwa namna gani kila shughuli ina umuhimu wake na inatambulika ndani na nje ya nchi ilimradi haivunji sheria za nchi.

Pia unaweza kuona hata katika tuliotajwa kuwania kipengele cha dansa bora Afrika 2021, mwanamke nilikuwa peke yangu. Nasisitiza wasichana wasimamie, wafanye kwa bidii kile wanachokiamini, wasikatishwe tamaa.


Swali: Unadhani kwa nini wazazi hawawapi nafasi vijana au mabinti zao kujikita kwenye sanaa?

Angel Nyigu: Kuna dhana kuwa sanaa ni uhuni, labda kwa sababu ya muda unaofanyika mara nyingi ni usiku, mavazi na mchanganyiko kwa maana ya wasichana na wavulana kuwa pamoja muda mwingi, lakini kiuhalisia uhuni, tabia mbaya, kuvaa nusu utupu, kujisitiri na mengine kama hayo ni tabia ya mtu.

Kama mtu ana tabia mbaya hata akifungiwa ndani atatafuta namna ya kutoroka na kwenda kufanya uovu wake.

Narudia sanaa siyo uhuni, bali ni maisha na ukiwa msanii hilo linaonekana hata katika maisha yako halisi, kama mimi ninadansi si rahisi kuvaa sketi ndefu halafu niruke juu au niinue mguu juu, ukitafsiri uhuni katika muktadha huo nitaona unanionea, nawe utajiona upo sahihi. Ndiyo maana ninasema ni mtazamo wa mtu.


Swali: Unawaambiaje wazazi kuhusu sanaa na watoto wao?

Angel Nyigu: Wawape nafasi, sanaa ni maisha, muhimu wao kuchagua waishi vipi na wawape burudani ipi wengine wanaoishi pamoja nao.


Swali: Mbali na kujituma, nini kimekusaidia kufika hapo ulipo?

Angel Nyigu: Dah...ukiachilia watu wanaoniunga mkono kwa kuhitaji huduma yangu kwenye kazi zao za muziki, mitandao ya kijamii ndiyo kila kitu. Hata watu wengi wamenijua kupitia mitandao na kazi zangu pia zinaonekana huko.


Swali: Unajivunia nini tangu uwe dansa?

Angel Nyigu: Kikubwa nimetambulika, pia nimefungua darasa.

Hapa ninaongeza kipato changu kwa sababu sifundishi bure, wananilipa kulingana na tulivyokubaliana.

Lengo langu ni kuja kuwa na chuo kikubwa kitakachotambulika ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kufundisha madansa namna ya kushambulia jukwaa na kunengua.