Askofu Gwajima ashukiwa kwa kupinga chanjo

Balozi wa Marekani nchini Tanzania,Dk. Donald Wright (kulia) akikabidhi sehemu ya mzigo wa chanjo ya  homa ya Corona nchin (Covid 19)  kwa Waziri wa Afya Dk Doroth Gwajima  mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.Katikati ni  Waziri wa Mambo ya nje Balozi Liberata Mulamula .Na mpiga picha wetu

Muktasari:

  • Viongozi wa dini na wanasiasa wamemkosoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa kauli yake ya kupinga matumizi ya chanjo za maambukizi ya Covid 19, huku CCM ikionya tabia ya makada wake kupinga kauli za viongozi wao.

Dar/Mikoani. Viongozi wa dini na wanasiasa wamemkosoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa kauli yake ya kupinga matumizi ya chanjo za maambukizi ya Covid 19, huku CCM ikionya tabia ya makada wake kupinga kauli za viongozi wao.

Kauli za Askofu Gwajima ambaye pia ni mbunge wa Kawe zimekuja siku moja baada ya Serikali kupokea awamu ya kwanza ya msaada wa dozi 1,058,400 za chanjo dhidi ya virusi vya corona, huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorthy Gwajima akiwahakikishia Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama kwa matumizi, hivyo wajitokeze kuchanjwa.

Akizungumza juzi katika ibada iliyofanyika katika kanisa hilo lililopo Ubungo- Kibo, Dar es Salaam, Askofu Gwajima aliwaonya wataalamu wa afya wanaoshadadia wananchi kuchanjwa chanjo hizo.

“Mimi namtaka daktari atakayeshadadia nitakula naye meza moja. Utakufa daktari, utaona,” alisema Askofu Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake.

Aliendelea: “Daktari yoyote wa Kitanzania atakayeanza kushadadia watu wachanjwe na yeye mwenyewe hajafanya utafiti wa kuna nini ndani ya chanjo, madhara ya muda mfupi, madhara ya muda mrefu kwetu na watoto wetu na nchi yetu. Nasema hivi kufa na ufe kwa jina la Yesu.”

Baada ya kauli hiyo ya Askofu Gwajima kusambaa katika mitandao ya kijamii, baadhi ya viongozi wa siasa na dini wamempinga akiwemo Mbunge wa Bumbuli, January Makamba aliyeandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Kauli ya Askofu Gwajima kuhusu chanjo na dhamira ya Serikali kuileta nchini haikubaliki, ni hatari kupotosha watu wanaotuamini kuhusu mambo ambayo hatuna utaalamu nayo, mjadala kuhusu usalama wa chanjo ni sahihi, lakini kiapo kwamba Serikali imeileta kuwadhuru watu si sahihi.”

Naye Mbunge wa zamani wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa amenukuliwa katika video iliyosambaa mitandaoni akiitaka Serikali kumchukulia hatua Askofu Gwajima akisema atasababisha Watanzania wengi wafe kwa upotoshaji wake.

“Ningemsihi (Askofu Gwajima) aheshimu taaluma za watu akawasikiliza wataalamu. Kitendo cha kusema wale wote wanaopigia chapuo dawa hizi wamepewa pesa maana yake anamtuhumu hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndiye mwenyekiti wa chama chake,” alisema Mchungaji Msigwa.


CCM yaonya

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu ilisema chama hicho kinafuatilia kwa makini mienendo ya baadhi ya viongozi wake wanaopotisha umma na kwenda kinyume na maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu na maadili ya chama.

Hata hivyo, taarifa ya CCM haijataja jina la mtu anayeonywa.

“CCM inawahakikishia wanachama na Watanzania kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wote wanaotumia nafasi hiyo kusukuma ajenda zao binafsi, kwa mujibu wa Katiba, kanuni za maadili na uongozi za CCM,” ilieleza taarifa ya chama hicho.

Mbali na wanasiasa na viongozi wa dini, Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amemtaka Askofu Gwajima afanye kazi ya kuhubiri na aachane na madaktari pamoja na wataalamu wa sayansi. “Yeye siyo daktari akitaka kuwa daktari aje tu shule. Kuna chanjo nyingi na dawa tunazitoa kwa wagonjwa amewahi kuuliza zinafanyaje kazi?

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliunda kamati ya wataalamu wa juu kabisa kwenye eneo la chanjo nchini na wamekuja na mapendekezo mazuri ya kisayansi. Cha kushangaza Askofu Gwajima anaachwa tu kupotosha umma,” alisema Dk Osati.

Dk Osati alisema umefika wakati Serikali kuja na mkakati mzuri wa kukaa na makundi mbalimbali kama viongozi wa dini, makundi ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa, wafanyakazi, wanahabari, ili waelewa dhana nzima ya chanjo na faida zake.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe alisema alichokisema Gwajima ajue anapingana na Mwenyekiti wa chama chake cha CCM.

“Aliyesema chanjo zije ni bosi wake kisiasa. Inafaa ajiuzulu siasa. Pili, atofautishe dini na sayansi. Ahubiri imani ya kuwapeleka watu mbinguni,” alisema Dk Mwaibambe. Hadi mwisho wa wiki iliyopita, taarifa ya Serikali ilisema Tanzania ilikuwa na jumla ya wagonjwa 858 na vifo 29.


Mwitikio hafifu wa wananchi

Ikiwa ni siku moja tangu Serikali ilipotoa mwongozo wa 17 wa kukabiliana na maambukizi ya Covid 19, Mwananchi limebaini mwitikio hafifu wa wananchi.

Mwongozo huo ulitolewa juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi akisema ni lazima mtu kuvaa barakoa katika vyombo vya usafiri na stendi za mabasi, daladala na bodaboda, huku ikiviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti bila kusimamisha abiria.

Maeneo kama soko la Shekilango, Sinza na hata Stendi ya Makumbusho, watu walionekana wakiendelea na shughuli zao kama kawaida bila kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo, jambo linalohatarisha maisha yao. Hali hiyo imeonekana si tu kwa mtu mmoja mmoja, bali hata wamiliki wa biashara bado hawajawa mwamko wa kuweka maji tiririka na sabuni kwa ajili ya wateja wanaowahudumia ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga na virusi hivyo. “Unaweza kuwa na maji, lakini mtu hanawi, tulichofanya sisi tumeweka vitakasa mikono mlangoni na mtu haruhusiwi kuingia bila kutumia,” alisema Daniel Mushi, mfanyabiashara eneo la Kunduchi.

Mkoani Tanga baadhi ya maelekezo yameanza kufuatwa kwa baadhi ya kampuni za mabasi yaendanyo mikoani, lakini daladala zimeendelea kujaza abiria kama kawaida.

Mwananchi ilipita katika ofisi ya kukatia tiketi ya kampuni ya mabasi ya Tashriff iliyopo barabara ya 14 jijini Tanga na kukuta mfanyakazi wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Awadh akiwatangazia abiria kwa kutumia kipaza sauti kuhusu kila mmoja kuvaa barakoa na kuwa na kitakasa mikono.

Ofisa wa mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa nchi kavu (Latra) mkoa wa Tanga, Kenedy Jakabondo alisema leo (jumanne) maofisa watapita katika vituo vyote vya mabasi kutangaza kuhusu mwongozo wa kujikinga na corona kwa kutumia gari.

Mkoani Kilimanjaro nako kumekuwa na mwitikio hafifu, kwani abiria wameonekana kutozingatia maelekezo ya Serikali.

Jana na juzi, Kaimu Ofisa wa Latra mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Umoti kwa kushirikiana na wasafirishaji na Jeshi la polisi walikuwa wakizuia mabasi kutoka katika kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi kama kuna abiria hajavaa barakoa.

“Jana (juzi) tulikuwa kwenye mageti yote ya kutoka stendi kuhakikisha hakuna basi linatoka kama wahudumu na abiria hawajavaa barakoa. Leo (jana) niko hapa stendi mimi mwenyewe kuhakikisha tahadhari za corona zinachukuliwa,” alisema.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Yuvenal Theophil, Burhani Yakub, Mussa Juma, Harriety Makweta na Aurea Simtowe