‘Baba’ wa Diamond Platnumz aeleza haya

‘Baba’ wa Diamond Platnumz aeleza haya

Muktasari:

  • Baada ya kuelezwa kuwa Abdul Jumaa si baba mzazi wa msanii wa Bongo fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, mzee huyo amesema anaamini kuwa yeye ndio baba mzazi wa mkali huyo wa wimbo wa Waah aliomshirikisha mwanamuziki Koffi Olomide.

Dar es Salaam. Baada ya kuelezwa kuwa Abdul Jumaa si baba mzazi wa msanii wa Bongo fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, mzee huyo amesema anaamini kuwa yeye ndio baba mzazi wa mkali huyo wa wimbo wa Waah aliomshirikisha mwanamuziki Koffi Olomide.

Jana Ijumaa Januari 15, 2020 mama mzazi wa msanii huyo,  Sanura Kassim, maarufu mama Dangote, alitoa taarifa ya kutikisa mitandao ya kijamii kwamba mzee Abdul si baba halisi wa Diamond, bali ni baba mlezi.

Mama huyo alisema baba mzazi wa msanii huyo ni Salum Iddy Nyange ambaye ni marehemu.

Leo wakati akihojiwa na televisheni mtandao ya Zamaradi, Abdul amesema anafahamu kuwa Diamond ni mwanaye.

 “Nimeshukuru nami nimepata uhakika sio mbaya, na mimi nashukuru kweli sio baba yake basi ni hilo tu naweza kutamka maana sikupata mshtuko sana kwa sababu sio msiba au kusema ni mtu alikuwa na mategemeo sana kwangu kupita kiwango, hapana.”

“Diamond ni mwanangu toka mimba maisha tuliyoishi  mpaka nampeleka hospitali, mpaka nakuja kumpokea hospitali namtoa mpaka narudi tunaanza maisha mpaka nakuja kukorofishana na mama yake,” amesema mzee huyo.

Huku akieleza kuwa hakuwahi kusikia akielezwa kuwa msanii huyo si mwanaye amesema, “mimi nipo naye sijawahi kusikia neno la aina yeyote au mama kuzungumza au kumwambia mtoto wakati ule anasoma bwana huyu sio baba yako au huyu sio mama yako.”

“Mpaka leo hili linakuja kutamkwa neno hili na mdomo sahihi kabisa ndio naamini kuwa mimba sio yangu lakini mimi naamini mimba ni yangu.”

Amesema licha ya kuelezwa kuwa si baba halisi wa msanii huyo na kwamba alikana ujauzito amesema suala hilo si kweli, “...,baba mlezi halafu baba aliikataa mimba, sasa itakuaje nikatae mimba halafu nimlee mtoto.”

Amesema alitengana na mama Dangote wakati Diamond akianza kidato cha kwanza, “hata jina la Naseeb mimi ndio nilimpa.”