‘Bajeti inayotekelezeka ni ya kununua mashangingi’

Muktasari:

  • Ununuzi wa magari ya kifahari maarufu kwa jina la Mashangingi kwa ajili ya kuwaendesha viongozi wa Serikali, umeonyesha kuwakera baadhi ya wananchi wakihoji sekta muhimu kutofikishiwa fedha zote zilizopangwa katika bajeti.

Dar es Salaam. Ununuzi wa magari ya kifahari maarufu kwa jina la Mashangingi kwa ajili ya kuwaendesha viongozi wa Serikali, umeonyesha kuwakera baadhi ya wananchi, akiwamo Ismail Mohammed, aliyedai kuwa ndio mahali pekee ambapo Serikali huwekeza fedha za kutosha huku, maeneo mengine muhimu yakiwa na upungufu.

Mohamed ameyasema hayo leo Jumatano Juni 7, 2023 katika mjadala wa Twitter Space unaoendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communicationi, uliobeba mada ya ‘Matarajio Bajeti za kisekta zilizopitishwa na Bunge zinakidhi mahitaji ya wananchi?’

“Kila mwaka unakuta bajeti nyingine zimeporomoka chini ya asilimia 50, unajiuliza kwa nini wao ndio wanazitenga hizo bajeti lakini hawazitekelezi lakini zile za kununua magari zinatekelezeka,” amhoji mwananchi huyo.

Aidha Mohamed amesema bajeti ingepaswa kuangalia sekta muhimu ikiwemo kilimo, afya na elimu kwani ukiangalia mwaka ulioisha chakula kilipanda bei na yote ni kwa sasa babu bajeti hawafikii wakulima wa chini ikiwemo ununuzi wa pembejeo.

“Nchi ya Zambia utakuta Waziri wa kilimo wanatembelea gari la kawaida wala hana V8, lakini ndio wanalima sana, lakini hawa wa kwetu wanaotembelea magari ya kifahari, ule utekelezaji wa kilimo bado ni sifuri,” amesema.

Akichangia mjadala huo, Katibu kiongozi Baraza Kivuli la Mawaziri wa chama cha ACT, Idrissa Kweweta, amesema katika kila bajeti kuna upungufu wa fedha zilizowekwa ukilinganisha na mahitaji na maeneo mengine kuwa na matundu kwa kutojibu mahitaji ya wananchi kwa ujumla wake.

Kweweta ametoa mfano katika Wizara ya kilimo ambayo Serikali imejipanga kufanya mageuzi makubwa, lakini bado kuna changamoto ikiwemo uwiano wa bajeti ya kilimo na uwiano wa bajeti ya kuu ya Serikali.

“Mfano kwa miaka mitatu mfululizo, mwaka 2021/22 bajeti ya kilimo ilikuwa Sh630 bilioni, lakini ukiangalia uwiano wa fedha hizo na uwiano bajeti ya serikali ilikuwa ni asilimia 1.7.

Amesema hilo linatokea wakati nchi imeingia makubaliano ya Malabo ya walau kutenga bajeti ya walau asilimia 15 ya bajeti ya serikali ya kilimo ili kuhakikisha kilimo kiweze kukua kwa wastani wa asilimia nane ambayo ni malengo serikali imejiwekea.

“Tunaona Serikali imeweka malengo, lakini utekelezaji wa bajeti yake hauendi kujibu malengo hayo na ndio maana unaona kasi ya kilimo inapungua.

“Mfano kwa mwaka juzi kilimo kilikuwa kinakuwa kwa asilimia 2.8, mwaka unakuta huu kimeshuka hadi kufika asilimia 2.2,” amesema.